IQNA – Shirika la Kitaifa la Vyombo vya Habari la Misri limetangaza kuzinduliwa kwa kipindi kipya chenye kichwa cha habari “Imam Mkuu”, kilichotengwa mahususi kwa ajili ya hotuba na mawaidha ya Maimamu wa Al-Azhar katika miongo kadhaa iliyopita.
Shirika hilo, likiongozwa na Ahmed Moslamani, lilitangaza uzinduzi wa kipindi hicho.
Kipindi hicho kitajumuisha hotuba na mawaidha yaliyotolewa na Masheikh na Maimamu wa Al-Azhar katika kipindi cha miaka 90 iliyopita. Kitashughulikia kipindi cha uongozi wa Al-Azhar kuanzia wakati wa Sheikh Muhammad Mustafa el-Maraghi hadi Sheikh Ahmed el-Tayeb, Imam Mkuu wa sasa wa Al-Azhar.
Abdel Rahman Bassiouni, Mkuu wa Redio ya Misri, alieleza kuwa kipindi hicho kitajikita kwenye hotuba za Masheikh wa Al-Azhar walioshikilia wadhifa huu katika karne ya 20 na 21.
Ismail Douidar, Mkuu wa Mtandao wa Idhaa ya Qur’an ya Misri, alisema kuwa kituo hicho kina hifadhi kubwa ya mihadhara ya Masheikh hawa mashuhuri, iliyorekodiwa kabla na baada ya kuanzishwa rasmi kwa kituo hicho cha redio.
Aliongeza kuwa kituo hicho kimefanya mawasiliano na wakusanyaji wa urithi wa Kiislamu na rekodi adimu ili kupata kanda zozote walizonazo kutoka enzi ya utangazaji wa binafsi, ili kuzijumuisha katika kipindi hicho ikiwezekana.
Hifadhi ya redio hiyo inajumuisha takriban mihadhara 600 iliyorekodiwa ya Maimamu mashuhuri wa Al-Azhar. Mihadhara hii inajumuisha 180 ya Sheikh Ahmed Al-Tayeb, 99 ya Sheikh Jad Al-Haq Ali Jad Al-Haq, 92 ya Sheikh Muhammad Sayyed Tantawi, 90 ya Sheikh Mahmoud Shaltout, 64 ya Sheikh Abdul Halim Mahmoud, 38 ya Sheikh Hassan Maamoun, 20 ya Sheikh Abdul Rahman Al-Bisar, na mihadhara miwili ya Sheikh Muhammad Mustafa Al-Maraghi, ambayo ilirekodiwa wakati wa enzi ya utangazaji wa binafsi wa redio hiyo zaidi ya miaka 92 iliyopita.
4369976