IQNA – Mashindano ya Qur'ani ya kila mwaka ya “Al-Rasoul Al-Aazam” (Mtume Mtukufu SAW) yamefunguliwa katika mji mkuu wa Yemen, Sana’a, siku ya Jumapili kwa mnasaba wa Milad un Nabii.
Shule za Kizazi cha Qur’an, chini ya Kitengo cha Utamaduni cha Mamlaka ya Wanawake katika Sekretarieti ya Mji Mkuu, zimezindua mashindano hayo kama sehemu ya sherehe za kuadhimisha kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (SAW) yaani Milad un Nabii.
Karibu wanafunzi 500 wa kike kutoka Shule mbalimbali za Kizazi cha Qur’an wanashiriki, huku wanafunzi 170 wakifuzu kwa raundi za ngazi ya wilaya na hatimaye fainali za Sekretarieti ya Mji Mkuu.
Ofisa mmoja wa mashindano hayo, Bi. Sima Muayad, alisema kuwa hafla hiyo ni sehemu ya shughuli za kila mwaka za kuadhimisha kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (SAW) na inalenga kulea kizazi chenye msingi imara wa elimu ya Qur’an na kilichojitolea katika mafundisho ya Mtume Mtukufu (SAW).
Alibainisha kuwa mashindano hayo yanatoa jukwaa la kielimu na kiroho la kubainisha na kuhamasisha wanafunzi bora katika kuhifadhi Qur’an. Raundi za mchujo zitaendelea hadi mashindano ya fainali, yakikutanisha wanafunzi kutoka wilaya zote.
Aliongeza kuwa mashindano hayo yanatafuta kuimarisha utamaduni wa Qur’an, kuongeza uelewa wa wasifu wa Mtume (Seerah) miongoni mwa vizazi vichanga, na kuunganisha sherehe za kuzaliwa kwa Mtume na elimu, vitendo, na kumfuata Mtume Muhammad (SAW) kama kielelezo chema.
3498674