Kwa mujibu wa gazeti la Al Anwar, Allamah Fadhlullah amesema hayo alipokutana na Ujumbe kutoka Chuo Kikuu cha Imam Khomeini nchini Iran. Mwanachuoni huyo ameashiria jinai za utawala haramu wa Israel katika eneo la Mashariki ya Kati na kusema kuwa: "Kwa kuzingatia maafa aliyosababisha Shimon Perez (Rais wa Israel) na hasa amri ya kuwaua raia waliokuwa wamekimbilia makao ya Umoja wa Mataifa nchini Lebanon na vile vile kutekeleza ukatili huko Qana, basi kwa hakika hakuna shaka kuwa yeye ni mtenda jinai"
Mkutano uliopewa jina la Utamaduni, Amani na Mazungumzo Kati ya Dini ulianza kazi zake jana huko New York katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa. Mkutano huo uliotayarishwa na Saudi Arabia ulitoa fursa kwa utawala haramu wa Israel kuzungumzia suala la amani wakati askari wake wakiendelea kuwaua kinyama wananchi wasiokua na hatia wa Palestina. Rais wa utawala ghasibu wa Israel Shimon Perez alipewa fursa ya kuzungumzia amani katika mkutano huo wakati Umoja wa Mataifa ukitahadharisha juu ya hali mbaya na mashaka makubwa ya raia zaidi ya milioni moja wa Ukanda wa Gaza na kutaka walimwengu wafanye juhudi za kuvunja mzingiro wa Wazayuni dhidi ya eneo hilo.
Mfalme Abdullah bin Abdulaziz wa Saudi Arabia alihutubia mkutano huo bila hata ya kuashiria jinai za Israel huko Palestina akizungumzia masuala ya wazi ya kidini na umuhimu wa mazungumzo kati ya dini mbalimbali. Mkutano huo unahutubiwa na rais anayeondoka wa Marekani George Bush ambaye ametambuliwa na Wamarekani wenyewe kuwa ndiye kiongozi mbaya na anayechukiwa zaidi katika historia ya Marekani.
Saudi Arabia imelaumiwa na duru za kutetea haki za binadamu na za kidini kwa kumwalika Rais na Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel katika mkutano huo.
Wakati huo huo Nawaf Musawi mkuu wa masuala ya kimataifa katika harakati ya Hizbullah ya Lebanon amekosoa mpango wa Saudi Arabia kuhusu kongamano hilo la utamaduni, amani na mazungumzo kati ya dini na kusema, lengo kuu la mkutano huo ni kulazimisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni. Amesema, la kushangaza ni kuwa mmoja kati ya wazungmzaji katika mkutano huo unaofanyika katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa (Shimon Perez) ni mbaguzi na katili aliyetekeleza jinai ambazo hazijawahi kushuhudiwa. Amesema, mahala anapopaswa kupelekwa Perez ni Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu ili ahukumiwe kwa ajili ya jinai zake dhidi ya Wapalestina na Walebanoni.
Harakati ya kupigania ukombozi wa Palestina ya Jihad Islami pia imelaani kikao hicho cha New York. 319581