IQNA

11:23 - November 26, 2008
Habari ID: 1712904

Kikao cha kimataifa cha ‘Vijana wa Ulimwengu wa Kiislamu’ mjini Tunisia

Kikao cha kimataifa cha ‘Vijana wa Ulimwengu wa Kiislamu, Fursa Zilizopo na Changamoto za Baadaye’ kilianza siku ya Jumatatu huko mjini Tunis Tunisia, kwa kuhudhuriwa na Ayatullah Muhammad Ali Taskhiri, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha pamoja Madhebu za Kiislamu.

Kwa mujibu wa shirka rasmi la habari la Imarati Awam, kikao hicho kimeandaliwa na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Nchi za Kiislamu Isesco, na kuandaliwa na idadi kubwa ya shakhsia wa Kiislamu na kimataifa. Wawakilishi wa Umoja wa Mataifa, Benki ya Kimataifa ya Ustawi, Mfuko wa Umoja wa Kimataifa wa Ustawi wa Jamii na wawakilishi wa mashirika kadhaa ya kisiasa, kiutamaduni, kijamii na kiuchumi ya nchi za Kiislamu ni miongoni mwa washiriki wa kikao hicho. Rais Zeinul Abidin bin Ali, wa Tunisia ambaye alitoa hotuba ya ufunguzi wa kikao hicho amesema kuwa nchi za Kiislamu zinapasa kuzingatia zaidi masuala ya vijana na kuwazuia wasitumbukie katika mtego wa makundi yenye misimamo mikali na ya kupindukia mpaka. Washiriki wa kikao hicho wametaka mwaka 2010 kutajwa kuwa ‘mwaka wa kimataifa wa vijana’ na kuandaa vikao kadhaa vya kuchunguza matatizo ya vijana na changamoto za kifikra zinazowahusu. Elimu na malezi ya vijanana kuwaandalia fursa za ajira, kuwalea kwa msingi wa thamani za Kiislamu zikiwemo za kusamehe na kukubali fikra za upande wa pili, kuishi pamoja kwa amani, kushajiisha mazungumzo baina ya tamaduni na ustaarabu tofauti ni miongoni mwa masuala yatakayojadiliwa katika kikao hicho. Vilevile kuchunguzwa chanzo cha mitazamo ya kufurutu mipaka, utumiaji nguvu na fikra potofu miongoni mwa vijana wa madhehebu mbalimbali katika ulimwengu wa Kiislamu na kutafuta njia za kukabiliana na fikra hizo, fursa na changamoto za utandawazi katika umma wa Kiislamu na kuwashirikisha vijana katika maisha ya kisiasa, kiutamaduni, kijamii, kimasomo na mahubiri ya kidini ni maidhui nyingine zitakazopewa umuhimu katika kikao hicho. Washiriki wamesisitiza kufunzwa vijana kwa msingi wa mafundisho na thamani za Kiislamu na kuwaepusha na fikra potofu na za kupindukia mipaka. Ayatullah Taskhiri, akiwa mwakailishi wa Jamhuri ya Kiislamu katika kikao hicho ametoa hotuba ambayo imezungumzia jinsi vijana wa Kiislamu wanavyopasa kupewa mafunzo kwa msingi wa matakwa ya Mtume Mtukufu (saw). Kikao hicho ambacho kinafanyika kwa udhamini wa Isesco na serikali ya Tunisia kitaendelea kwa muda wa siku tatu. 325516
captcha