IQNA

11:05 - November 27, 2008
Habari ID: 1713189

Misri yakosoa upinzani wa magharibi dhidi ya azimio la kuzuia kutusiwa dini

Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri Ahmad Abul Gheit amekosoa vikali nchi za Magharibi zikiongozwa na Umoja wa Ulaya na Marekani kwa kupinga mpango wa nchi za Kiislamu wa kukabiliana na kutusiwa na kuvunjiwa heshima dini.

Kwa mujibu wa gazeti la Misri la Al Akhbar, Ahmad Abul Gheit amesema: “Upinzani wa nchi za Magharibi kwa uamuzi huu wa nchi za Kiislamu kwa mara nyingine unabainisha kutozingatia jamii za Maghairbi matatizo ya Waislamu waliowachache katika nchi za Magharibi kama vile ubaguzi wa rangi na utumiwaji mabavu dhidi yao”.
Ameongeza kuwa, Jamii za Kimagharibi zinatetea matusi dhidi ya dini na kuvunjiwa heshima matukufu ya kidini kwa kisingizio cha uhuru wa maoni na itikadi. Hii ni katika hali ambayo kanuni za kimataifa na taasisi za kisheria zinapinga uzushaji chuki na ubaguzi dhidi ya wafuasi wa dini nyinginezo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri amesema kuwa mpango wa nchi za Kiislamu wa kupambana na wanaotusi dini haumaanishi kupinga uhuru wa maoni bali lengo lake ni kuzitaka nchi zote duniani kuchukua hatua dhidi ya wabaguzi wa rangi wanaotumia mabavu na wanaotusi na kuzivunjia heshima dini. Ameongeza kuwa, kutusi na kuvunjia heshima si tu kuwa kunakosa kuheshimu uhuru wa maoni, bali pia kunakiuka haki za kidini na ibada.
Itakumbukwa kuwa rasimu ya azimio la kupambana na matusi na kuvunjia heshima dini liliwasilishwa na nchi za Kiislamu tarehe 25 November mbele ya Kamati ya Haki za Binaadamu ya Umoja wa Mataifa na kupasishwa kwa kura 85 za ndio, kura 50 za hapana na kura 42 zisizopendelea upande wowote. 326382

captcha