IQNA

Kuanza kikao cha Baraza la Wanawake wa Kiislamu wa Afrika

14:38 - November 29, 2008
Habari ID: 1713845
Kikao cha siku mbili cha Baraza la Wanawake wa Kiislamu kilimaliza shughuli zake jana katika mji mkuu wa Mali, Bamako. Kikao hicho kimesimamiwa na Baraza la Mipango la Umoja wa Mataifa kwa Ajili ya Ustawi wa Kiutamaduni.
Mwakilishi wa baraza hilo Joseph Byll-Cataria amesema katika sherehe za ufunguzi wa kikao hicho kwamba lengo lake ni kukuza kiwango cha utamaduni wa wanawake na kuimarisha nafasi ya wanawake wa Kiislamu katika masuala ya kijamii, kiutamaduni na kisiasa kwa ajili ya kuwawezesha kukabiliana na matatizo ya jamii ya mwanadamu. Byll-Cataria ameongeza kuwa zinafanyika juhudi za kukuza vipawa vya wanawake wa Afrika na kudhihirisha mchango wao katika jamii.
Waziri wa Masuala ya Wanawake, Watoto na Familia wa Mali Maiga Sina Damba amesisitiza katika kikao hicho juu ya udharura wa kupewa umuhimu zaidi mchango wa wanawake wa Kiislamu barani Afrika na akasema kuwa wanawake wa Afrika wanapewa nafasi ndogo katika kuainisha masuala muhimu ya jamii zao na hawashirikishwi ipasavyo katika masuala ya kisiasa na kijamii.
Sina Damba amesema kuwa wanachama wa Baraza la Wanawake wa Kiislamu wa Afrika wataanzisha ushirikiano wa kudumu na wawakilishi wa nchi za Umoja wa Afrika, Jumuiya ya Nchi za Kiislamu OIC na Baraza la Mipango l Umoja wa Mataifa kwa Ajili ya Ustawi wa Kiutamaduni.
Kikao cha Baraza la Wanawake wa Kiislamu wa Afrika kimehudhuriwa na wawakilishi wa jumuiya mbalimbali za Kiislamu ikiwemo Jumuiya ya Nchi za Kiislamu OIC. 326905

captcha