Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu IOC, amewatumia Waislamu wote duniani salamu za pongezi na fanaka kwa mnasaba wa kuwadia sikukuu ya Idul Adh'ha. Katika ujumbe alioutoa kwa mnasaba huo, Ekmeleddin Ihsanoghlou amewatakia Waislamu amani na utulivu wa kudumu maishani.
Akibainisha umuhimu wa siku hii adhimu, Ihsanoghlou amesema kuwa Idul Adh'ha ni moja ya idi kubwa za kidini za Waislamu na iliyo na maana kubwa kwao, ikiwemo ya kumtii na kumwabudu Mwenyezi Mungu kwa moyo mkunjufu. Amesema idi hiyo ni fursa muhimu kwa Waislamu kukusanyika pamoja katika msimu wa ibada tukufu ya hija na kwamba, inaweza kuwa na maana maalumu na muhimu ya umoja na mshikamano kwa Waislamu ambao wanakutana kwa pamoja katika mlima wa Arafa. Ameendelea kusema kuwa hija ni fursa muhimu kwa Waislamu kukusanyika pamoja na kutafuta njia za kutatua matatizo yao na vilevile mbinu za kuwawezesha kuimarisha umoja na mshikamano miongoni mwao, ili kuweza kukabiliana na njama za maadui wa Uislamu na vilevile kulinda na kutetea matukufu wa Kiislamu.
Mkuu huyo wa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu amesema kuwa, ni jambo la kuridhisha kuona kwamba taasisi muhimu za Kiislamu na nchi wanachama wa umoja huo wa OIC pamoja na umma mzima wa Kiislamu zinafuatilia lengo moja nalo ni la kuisaidia OIC iweze kutimiza mipango yake ya kisiasa na kidini, jambo litakaloimarisha hali ya kijamii ya Waislamu na kuzuia kukanyagwa kwa matukufu ya Kiislamu. Amemuomba Mwenyezi Mungu awawezeshe Waislamu kuishi kwa amani na kuweza kufikia malengo yao ya maendeleo na usalama wa kudumu katika ulimwengu wa leo. 330778