IQNA

10:41 - December 09, 2008
Habari ID: 1717402

Idul Adh'ha fursa nzuri ya zoezi la ustahimilivu Nigeria

Rais Umar Musa Yar'Adua wa Nigeria ametoa wito kwa Wanigeria, hasa Waislamu, kutumia vizuri fursa ya siku nne za mapumziko ya kitaifa ya Idul Adh'ha kuhimiza ustahimilivu, hasa baada ya machafuko ya hivi karibuni katika mji wa kati wa Jos.

Rais Yar'Adua ameelezea masikitiko yake kutokana na machafuko ya hivi karibuni nchini humo yaliyopelekea watu wengi kupoteza maisha yao. "Kuna haja ya kukabiliana na changamoto kwa umoja kwani changamoto hizo zimekuwa kizingiti cha ustawi wa nchi", amesema Yar'Adua katika ujumbe wake wa Idul Adh'ha.
Rais Yar'Adua aidha ametoa wito kwa Wanigeria wa dini zote kutumia sikukuu ya Id ul Adh'ha kama fursa ya kutafakari jinsi ya kukomesha ghasia za kidini na kimadhehebu huku wakiishi kwa maelewano.
Itakumbukwa kuwa mamia ya watu waliuawa na misikiti na makanisa kuchomwa moto mwezi Novemba katika ghasia zilizoibuka kati ya Waislamu na Wakristo katika mji wa Jos.
Nigeria ina idadi ya watu zaidi ya milioni 140. Waislamu ni zaidi ya asilimia 55 huku Wakristo wakikadiriwa kuwa takribani asilimia 40 ya watu wote nchini humo. Nchi hiyo ya Afrika Magharibi ni mwanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu OIC na vile vile ni kati ya nchi zinazouza mafuta ya petroli kwa wingi duniani. 331733
captcha