Akizungumzia kadhai hiyo, Amir Musawi, mkuu wa zamani wa Kitengo cha Utamaduni cha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Sudan na mtaalamu wa masuala ya kimataifa na Mashariki ya Kati ambaye pia ni mshauri wa masuala ya vyombo vya habari katika Taasisi ya Utamaduni na Mawasiliano ya Kiislamu amesema katika mahojiano maalumu na shirika la IQNA kwamba, wanazuoni wa al-Azhar hawana ushujaa wa kumkosoa Tantawi kwa sababu anachaguliwa na kusimamiwa moja kwa moja na serikali ya Misri. Musawi amesema kwamba, Tantawi hawezi kuvumilia ukosolewaji wa aina yoyote ile kutoka kwa wanazuoni wa chuo hicho kwa sababu amepewa uwezo mkubwa na serikali ya Cairo ambao unamruhusu kuwafukuza kazi wakosoaji wake au hata kuwafunga jela. Amesema, Sheikh huyo Mkuu wa al-Azhar anatekeleza mfumo mbaya wa udikteta katika chuo hicho cha Kiislamu.
Musawi ametolea mfano mwanazuoni Yusuf Qardhawi, Mkuu wa Muungano wa Kimataifa wa Wanazuoni wa Kiislamu ambaye mara kwa mara hutoa mitazamo yake kuhusiana na masuala tofauti ya Mashariki ya Kati na ulimwengu wa Kiislamu, lakini mara hii amechukua uamuzi wa kukaa kimya na kutosema lolote kuhusiana na hatua ya kuaibisha ya hivi karibuni ya Tantawi kumpa mkono katili Shimon Peres, rais wa utawala dhalimu wa Israel, utawala ambao unawachinja kinyama Wapalestina wasio na hatia katika ardhi zao unazozikalia kwa mabavu. Hatua hiyo imeamsha hasira kubwa ya Waislamu ulimwenguni. Hii ni katika hali ambayo, Qardhawi hana uhusiano mzuri na Tantawi na amekuwa akidai kuwa mpinzani mkali wa siasa za mabavu na za kujitanua za utawala haramu wa Israel katika Mashariki ya Kati.
Amir Musawi ameendelea kusema kuwa wanazuoni wa Kiislamu wanapasa kuwajibika na kumuuliza Qardhawi ni kwa nini amekaa kimya na kutosema lolote kuhusiana na kitendo hicho cha Tantawi ambacho kimelenga kuuza thamani za Kiislamu na mapambano ya wananchi madhlumu wa Palestina kwa utawala ghasibu wa Israel. Amesema kuwa kitendo cha Tantawi kumpa mkono waziwazi Peres na kisha kudai kuwa hakuwa akimjua, ni dharau kubwa kwa ulimwengu wa Kiislamu na muamko wa Kiarabu na Kiislamu na kusisitiza kwamba madai yake hayo ni mabaya zaidi kuliko kitendo chenyewe cha kumpa mkono Peres. Amesema, kitendo hicho kimedharau na kutusi utu na heshima ya wanawake, vijana, watoto na wazee wa Palestina wanaokabiliwa kila siku na jinai na unyama wa Wazayuni.
Amir Musawi amesema kuwa kutokana na kuwa serikali ya Misri ni muungaji mkono mkubwa wa utawala ghasibu wa Israel, ni wazi kuwa Tantawi naye ambaye anachaguliwa moja kwa moja na rais wa nchi hiyo na kuwa mtumishi wa serikali anafuata siasa hizohizo za kuunga mkono na kuboresha uhusiano wa Waarabu na utawala huo ghasibu. 332836