IQNA

Salamu za pongezi za kuzaliwa Nabi Issa (as)

15:36 - December 27, 2008
Habari ID: 1723258
Katibu Mkuu wa Jumuiya za Kiislamu barani Ulaya Muhammad Bashari amesema ni sawa Waislamu kutoa salamu za pongezi kwa Wakristo wakati wa kumbukumbu ya kuzaliwa Nabi Issa (as) kwani jambo hilo hukuza umoja na mashikamano baina ya wafuasi wa dini hizo mbili.
Kwa mujibu wa gazeti la Al-Watan la Saudi Arabia, Bashari amesema: Uislamu hauwakatazi Waislamu kuwapa Wakristo mkono wa pongezi wakati wa idi na sikukuu zao za kidini. Amesema kuwa, Uislamu unasisitiza juu ya maelewano na Wakristo. Ameongeza kuwa kuwapa Wakristo salamu za pongezi kwa mnasaba wa mwaka mpya wa Miladia kutasaidia kuleta maelewano na kupunguza chuki na uhasama wa kidini.
Muhammad Bashari ameashiria aya ya 13 ya surat Hujurat katika Qur'ani Tukufu isemayo: "… Na tumekujaalieni kuwa ni mataifa na makabila ili mjuane…". Amesema katika aya hiyo Mwenyezi Mungu anaashiria suala la amani na watu kujuana kama malengo yake ya kuumba wanadamu wa mataifa mbalimbali.
Katibu Mkuu wa Jumuiya za Kiislamu Ulaya amesisitiza kuwa Uislamu ni dini ya kustahamiliana na kwamba katika sheria za Kiislamu kuimarisha amani ni moja ya misingi mikuu ya uhusiano wa Waislamu na wafuasi wa dini nyinginezo. 338465
captcha