“Mazungumzo na Marekani kuhusu suala la nyuklia, na labda masuala mengine, yatagonga mwamba,” asema Ayatullah Khamenei Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ametoa kauli hiyo Jumatano usiku jijini Tehran wakati alipohutubia taifa akizungumzia masuala ya kitaifa, kikanda, na kimataifa. Katika sehemu ya mwanzo ya hotuba yake, Kiongozi alisisitiza matumizi mengi ya madini ya urani au uraniumu iliyorutubishwa, akieleza nafasi yake katika kilimo, viwanda, ulinzi wa mazingira na rasilimali asilia, afya na tiba, lishe, pamoja na utafiti na elimu. Akiweka wazi asili ya tasnia ya urutubishaji wa madini hayo ya sekta yanyuklia nchini Iran, Imam Khamenei alisema: “Hatukuwa na teknolojia hii, na wengine hawakuwa tayari kutimiza mahitaji yetu.
Lakini, kwa azma ya mameneja waaminifu kadhaa, pamoja na jitihada za viongozi na wanasayansi, tulianza juhudi hii zaidi ya miaka thelathini iliyopita. Leo tumefikia kiwango cha juu cha uboreshaji.” Kiongozi Muadhamu alieleza kwamba, ingawa baadhi ya nchi hurutubisha urani kwa kiwango cha asilimia 90 kwa ajili ya kutengeneza silaha za nyuklia, Jamhuri ya Kiislamu ina mwelekeo tofauti kabisa.
“Nchi zinazotaka kutengeneza silaha za nyuklia hurutubisha hadi asilimia 90. Kwa kuwa sisi hatuna haja ya silaha hizo na tumeamua kutokuwa nazo, tumepandisha kiwango hadi asilimia 60 tu,” alithibitisha. Imam Khamenei alisisitiza nafasi ya kipekee ya Iran: “Nchi kumi duniani zina uwezo wa kurutubisha uraniumu, na moja ni Iran ya Kiislamu. Nchi nyingine tisa zina mabomu ya nyuklia. Sisi hatuna bomu la nyuklia, na hatutakuwa nalo. Hatuna nia ya kutumia silaha za nyuklia, lakini tuna urutubishaji.” Akiashiria miaka mingi ya mashinikizo kutoka madola kibeberu, Kiongozi Muadhamu alisema kwa uthabiti: “Hatukuwahi kukubali shinikizo juu ya suala la urutubishaji, na hatutakubali kamwe. Vilevile, katika masuala mengine, tumekuwa thabiti na tutaendelea kuwa thabiti.”
Ayatullah Khamenei alisema: “Marekani inasema Iran isihusike na urutubishaji. Serikali zilizopita za Marekani zilishinikiza kuwa tusirutubishe kwenye kiwango cha juu, lakini hii ya sasa inasema: ‘Msiwe na urutubishaji madini ya uranium hata kidog.’” Kiongozi alieleza: “Hii inamaanisha jukumu kubwa ambalo tumelipigania kwa gharama kubwa na kwa shida nyingi lifutwe na kutupwa! Ni wazi, taifa lenye heshima kama Iran litamkataa kabisa mtu anayependekeza jambo hilo.”
Katika sehemu ya pili ya hotuba, Imam Khamenei alieleza ubatili wa mazungumzo na Marekani: “Marekani imeshaamua matokeo ya mazungumzo kwa mtazamo wake, ikitaka matokeo yawe kusitishwa kwa shughuli za nyuklia na urutubishaji wa madini ya uraniumu ndani ya Iran.” Alisema kushiriki katika mazungumzo hayo ni sawa na kukubali amri na shinikizo la upande wa pili. “Sasa, rais wao anasema urutubishaji lazima ukome, na siku chache zilizopita mmoja wa maafisa wao alisema Iran isiwe na hata makombora ya masafa ya kati au mafupi , ikimaanisha mikono ya Iran ifungwe kiasi kwamba ikishambuliwa isiweze kujibu hata mashambulizi kwenye kambi zao.” Imam Khamenei alisema maneno haya yanadhihirisha kutokuelewa taifa la Iran na Jamhuri ya Kiislamu, pamoja na kutojua misingi na mwelekeo wake.
“Kauli hizi hazistahili kuzingatiwa; zinazidi hata hadhi ya msemaji.” Kiongozi alionya kwamba kukubali mazungumzo chini ya vitisho kunamaanisha kusalimu amri na kuhamasisha madai yasiyo na kikomo. “Leo wanasema ukifanya urutubishaji tutachukua hatua; kesho, uwe na makombora au mahusiano na nchi fulani , au kutokuwa nayo , itakuwa sababu ya vitisho na shinikizo.” Ayatullah Khamenei alisema: “Hakuna taifa lenye heshima litakalokubali mazungumzo chini ya vitisho.”
Akirejelea makubaliano ya JCPOA yaliyotiwa saini miaka kumi iliyopita, Kiongozi alisema: “Tulikubaliana kufunga kituo cha uzalishaji wa nyuklia na kufuta au kupunguza malighafi tulizorutubisha, ili tuondolewe vikwazo. Leo, baada ya miaka kumi, si kwamba tatizo limeisha bali limeongezeka kwenye Baraza la Usalama na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki, IAEA.” Kiongozi Muadhamu alikumbusha mauaji ya shahidi General Soleimani na mashambulizi ya mabomu ya Marekani dhidi ya miundombinu ya Iran kama ushahidi kwamba hawawezi kuaminiwa. Alisisitiza: “Mazungumzo na Marekani kuhusu suala la nyuklia, na masuala mengine pia, ni kugonga mwamba.” Katika hitimisho, Imam Khamenei alisema maendeleo na usalama wa taifa yatapatikana tu kwa kuwa na nguvu katika nyanja zote , kijeshi, kisayansi, kiserikali na kimuundo. “Adui hatatoa vitisho tukijijenga vyema,” alisema.
Imam Khamenei alisisitiza zaidi kuwa mshikamano wa taifa ndiyo sababu kuu ya kushindwa kwa adui katika Vita vya Siku Kumi na Mbili vilivyolazimishwa. “Mauaji ya makamanda na watu muhimu yalilenga kuchochea machafuko nchini, hususan mjini Tehran, kwa kutumia mawakala wao; kuvuruga mambo ya taifa, kukihujumu kiini cha mfumo wa utawala, na hatimaye kuiondoa kabisa Dini ya Uislamu kutoka katika nchi hii.”
Ameongeza kuwa: “Mpango wa adui ulikuwa kueneza machafuko baada ya kuuawa makamanda, lakini kuchaguliwa haraka warithi, moyo wa juu wa Jeshi na uratibu wa serikali ni mambo ambayo yaliyeta umoja na kumshinda adui. Kipengele cha muhimu zaidi kilichoshindwa adui kilikuwa mshikamano wa taifa.” Alisisitiza umuhimu wa mshikamano huo kubaki na kuendelea kutoa athari kubwa. Kiongozi alieleza kuwa Iran ya leo ni ile ile Iran ya tarehe 12 na 13 Juni 2025, akibainisha: “Wakati huo, mitaa ilijaa wananchi wakipaza kauli zenye nguvu dhidi ya utawala wa Kizayuni uliolaaniwa na Marekani dhalimu, zikidhihirisha mshikamano wa taifa — mshikamano ambao bado upo na utaendelea kuwepo.” Akimalizia, Imam Khamenei alimkumbuka shahidi Sayed Hassan Nasrallah kama hazina kubwa kwa Uislamu, Ushia na Lebanon: “Kisa cha Hizbullah kinaendelea. Hizbullah isidunishwe. Hazina hii isiwe ispuuzwe kwani ni kitu chenye thamani kwa Lebanon na kwa Ulimwengu mzima wa Kiislamu.”
Chanzo Khamenei.ir
3494728