Abul Khair Muhammad Zubair, mwanazuoni ambaye anaongoza Kamisheni ya Mwelekeo Mmoja wa Pakistan inayojulikana pia kama Umoja wa Madhehebu za Kiislamu wa Pakistan, alitoa kauli hizo katika mahojiano na Shirika la Habari za Qur'ani la Kimataifa (IQNA) pembezoni mwa Mkutano wa 39 wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu uliofanyika Tehran mapema mwezi huu.
Ameeleza kuwa Umoja wa Madhehebu za Kiislamu wa Pakistan ni taasisi binafsi iliyoanzishwa kwa msaada wa madhehebu yote ya Kiislamu, na lengo lake kuu ni kuwaleta pamoja viongozi wa madhehebu hayo.
Akizungumzia hali ya Gaza, Zubair alisema kuwa vita vimewakosesha raha na kuwatia wasiwasi Waislamu kote ulimwenguni.
“Tangu kuanza kwa vita vya Gaza, watu wa Pakistan wameisukuma serikali yao ichukue msimamo na kudai msaada wa vitendo kwa Gaza,” alieleza.
Aliongeza kuwa wananchi wa Pakistan hufanya maandamano ya kila wiki kupinga jinai za utawala wa Israel dhidi ya binadamu katika Ukanda wa Gaza.
Zubair alitaja taifa moja kwa mchango wake wa kipekee: “Iran ndilo taifa pekee lililotoa msaada wa vitendo kwa Palestina na kutoa mashahidi wengi wa thamani katika njia hii,” alisema. “Tunahimiza nchi zingine pia zitoe msaada wa vitendo kwa Palestina.”
Mwanazuoni huyo alisisitiza kuwa umoja ni wa lazima kwa sababu tamaa za nguvu za Kizayuni zinaenea zaidi ya Palestina. “Waislamu lazima wasimame pamoja dhidi ya ukoloni wa Israel kwa sababu uvamizi wa Palestina si lengo pekee la Wazayuni; macho yao ya tamaa yapo kwenye nchi zote za Kiislamu,” alisema kwa msisitizo. “Kwa hiyo Waislamu wote lazima waungane dhidi ya uovu kamili.”
Aliongeza kuwa baadhi ya makundi potofu yamejaribu kuathiri watu nchini Pakistan, lakini wanazuoni wa nchi hiyo wanajitahidi kuyakabili. Amesema vitabu vingi vinavyopinga makundi hayo vimetafsiriwa kutoka Kiarabu na Kifarsi kwenda Kiwurdu ili kuelimisha vijana.
Zubair pia ametaja uhusiano wake wa muda mrefu na Iran, unaotokana na enzi za muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Marehemu Imam Khomeini (MA).
Katika kufafanua umuhimu umoja na udugu miongoni mwa Waislamu, alinukuu aya ya 103 ya Sura Al‑Imran:
“Na shikamaneni kwa Kamba ya Mwenyezi Mungu, nyote pamoja, wala msifarakane. Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu juu yenu mlipokuwa maadui, akaunganisha nyoyo zenu, hivyo kwa neema Yake mkawa ndugu. Na akakuokoeni kutoka Shimo la Moto wakati mlikuwa karibu kuangukia humo. Hivyo Mwenyezi Mungu anabainishia aya Zake ili mpate kuongoka.”
3494717