Akizungumza kama mgeni wa heshima katika Tamasha la Pili la Kimataifa la Farabi hapa mjini Tehran, Dakta Haddad Adel amesema kuwa, utamaduni wa Kiislamu unapasa kupatiwa maana mpya katika kukabiliana na utamaduni wa nchi za Magharibi, maana ambayo inapasa kuoana na mafundisho ya dini tukufu ya Kiislamu. Amesema kuwa kwa kuanzishwa serikali na dola la Kiislamu nchini Iran, lengo kuu ni kufikiwa utamaduni wa Kiislamu. Dakta Haddad Adel amesema kuwa Waislamu hawajatekeleza vyema utamaduni wao na kwamba mafundisho na elimu kama vile falsafa, irfani na maadili ya Kiislamu hayapasi kuhusishwa tu na historia ya Kiislamu bali yanapaswa kutekelezwa kivitendo katika maisha yao ya kila siku. Amesema lengo la mapinduzi ya Kiislamu halikuwa ni kuubadilisha tu mfumo wa kisiasa nchini bali ulikuwa ni utangulizi wa kufikiwa utamaduni na elimu huru ya ubinadamu. Akiashiria kwamba mwanzilishi wa mfumo wa Kiislamu nchini Iran Imam Khomeini (MA) alikuwa mjuzi mkubwa wa masuala yanayomuhusu mwanadamu na vilevile mafundisho ya Kiislamu, Haddad Adel amesema kuwa kabla ya Imam Khomeini kuchukua usukani wa kuliongoza kisiasa taifa hili mwanzo alikuwa muhadhiri katika vyuo vya kidini na mwalimu wa maadili ya kiutu na kidini nchini.2396890