IQNA

Kongamano la kimataifa la thamani za mazungumzo katika Uislamu

13:33 - January 05, 2009
Habari ID: 1727536
Kongamano la kimataifa la “Kuchunguza Thamani za Mazungumzo Katika Uislamu” limefanyika katika mji wa Qayrawan nchini Tunisia.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Saudi Arabia SPA, kongamano hilo limefanyika kwa hisani ya Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Jumuiya ya Nchi za Kiislamu ISESCO kwa mnasaba wa mji huo wa Qayrawan kuteuliwa kama mji wa utamaduni wa Kiislamu mwaka 2009.
Kongamano hilo limehudhuriwa na idadi kubwa ya wasomi na wanafikra wa ulimwengu wa Kiislamu ambao wamechunguza njia za kuimarisha mazungumzo katika Uislamu na kuimarisha suala hilo katika mfumo wa elimu wa jamii za Kiislamu kote duniani.
Washiriki pia wamechunguza nafasi ya kihistoria ya maulamaa wa Kiislamu katika mji wa Qayrawan katika kukuza na kuimarisha utamaduni na ustaarabu wa Kiislamu.
Baada ya mji wa Qayrawan kuteuliwa kuwa mji wa utamaduni wa Kiislamu mwaka 2009, serikali ya Tunisia ilitenga bajeti ya dola milioni mbili kwa ajili ya kukarabati athari za kihistoria pamoja na kuandaa tamasha na mikitano mbali mbali mjini humo.
Historia ya mji wa Qayrawan inarudi nyuma hadi mwaka 50 Hijria ( 670 Miladia) na ni kati ya miji ya kale zaidi ya Kiislamu duniani. Mji huo ulijengwa mwanzoni mwa ustaarabu wa Kiislamu. Qayrawan ni neno la Kifarsi lililoingizwa katika lugha ya Kiarabu na linamaanisha eneo la kuweka silaha, kukaa wanajeshi na mahala wanapojumuika watu wakati wa vita.
Mji wa Qayrawan uko kilomita 160 kusini mwa Tunis, mji mkuu wa Tunisia na ulikuwa na nafasi muhimu katika Jihad na kuutangaza Uislamu. Msikiti wa Aqaba ibn Nafi ni kati ya athari za kale zaidi za kihistoria mjini humo. 343725
captcha