IQNA

Bendera ya utamaduni wa Kiislamu yakabidhiwa kwa mji wa Qayrawan

10:33 - January 05, 2009
Habari ID: 1727698
Bendera ya utamaduni wa Kiislamu imekabidhiwa kwa mji wa Qayrawan nchini Tunisia baada ya mji huo kuchaguliwa kuwa mji mkuu wa utamaduni wa ulimwengu wa Kiislamu katika mwaka huu wa 2009.
Qayrawan imepokea bendera hiyo kutoka kwa mji wa Alexandria, Misri.
Kwa mnasaba huo, serikali ya Tunisia imepanga mikakati mbalimbali ya kudhihirisha utamaduni wa Kiislamu kwa kufanya makongamano, mikutano ya kimataifa, maonyesho, mashindano, michezo ya kuigiza, filamu za aina mbalimbali na mafunzo ya muda ya sanaa.
Moja ya mipango muhimu ya mji wa Qayrawan katika mwaka huu ni nyimbo na tungo za kisufii, maonyesho ya mavazi ya Kiislamu, maonyesho ya sanaa na mapambo ya Kiislamu na kadhalika.
Shirika la Sayansi, Elimu na Utamaduni la Jumuiya ya Nchi za Kiislamu (ISESCO) kila mwaka huchagua miji mitatu na kuiarifisha kama miji mikuu ya utamaduni ya ulimwengu wa Kiislamu. Mwaka huu wa 2009 miji ya Qayrawan Tunisia, Kuala Lumpur Malaysia na N’Djamena huko Chad ndiyo iliyotangazwa kuwa miji mikuu ya utamaduni ya ulimwengu wa Kiislamu.
Mji wa Qayrawan ulijengwa mwaka 50 Hijria (670 Miladia) na kwa msingi huo unahesabiwa kuwa moja ya miji mikongwe ya Kiislamu. Jina la mji huo lina asili ya lugha ya Kifarsi na lina maana ya sehemu yenye silaha, jeshi na mahala pa kukusanyika watu wakati wa vita.
Ujenzi wa mji huo uliambatana na mwanzo wa historia ya ustaarabu wa Kiislamu na ulikuwa na mchango mkubwa katika mapigano ya jihadi na kueneza dini ya Kiislamu.
Mji wa Qayrawan uko umbali wa kilomita 160 kutoka mji mkuu wa Tunisia, Tunis. 811598

captcha