Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Habari la Kiislamu, kamati ya marefa ya tuzo hiyo iliitunukia jumuiya hiyo zawadi ya dola laki mbili pamoja na nishani ya dhahabu inayoandamana na tuzo hiyo.
Jumuiya ya Fiqhi ya Qur'ani na Sunna za Mtume (saw) ya Misri ni jumuiya isiyo ya kiserikali ambayo inajihusisha na shughuli za kijamii na uhubiri wa Kiislamu nchini Misri na nchi nyinginezo duniani.
Khalid al-Faisal, Amir wa mji mtakatifu wa Makka na mkuu wa Kamati Andamizi ya Tuzo ya Mfalme Faisal amesema, sababu za ushindi wa jumuiya hiyo ni pamoja na kutegemea kwake Qur'ani Tukufu na sunna za Mtume (saw) katika shughuli zake za kuleta muamko wa Kiislamu, kuzuia hujuma za maadui dhidi ya Uislamu na Waislamu, utekelezaji wa mipango ya kijamii na kuwasaidia wahitaji katika nchi za Misri, Palestina na nchi nyingine za Kiislamu na vilevile nchi za Kiafrika na Asia.
Kamati hiyo pia imemtunukia tuzo ya lugha ya Kiarabu na fasihi, Abdul Aziz al-Mane', mwanafasihi katika Chuo Kikuu cha Mfalme Saud katika mji wa Riadh.
Watafiti 29 kutoka nchi 11 za Kiarabu, Kiislamu na Ulaya walichaguliwa kuwa watafiti bora wa Kiislamu ambao wameuhudumia Uislamu na kupewa zawadi nono kutokana na mchango wao katika Uislamu.
Tuzo ya Kimataifa ya Mfalme Faisal iliasisiwa mwaka 1977 na kila mwaka hutoa zawadi na tuzo kwa taasisi, jumuiya na shakhsia bora zaidi waliohudumia Uislamu na pia lugha ya Kiarabu. 355606