Maonyesho ya sanaa ya uchoraji yaliyopewa jina la "Bosnia Jana, Leo Gaza" yamefunguliwa katika mji wa Sarajevo huko Bosnia Herzegovina kwa shabaha ya kuonyesha jinai zilizofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukanda wa Gaza.
Msimamizi wa maonyesho hayo Nina Hajich amesema kuwa wasanii 15 wa Bosnia wataonyesha mabango ya sanaa za michoro inayoakisi mauaji ya wakazi wa Ukanda wa Gaza waliouawa katika mashambulizi ya siku 22 ya utawala wa Kizayuni wa Israel.
Amesema kuwa sehemu nyingine ya maonyesho hayo itahusu mabango yenye picha zinazoakisi woga wa wanawake na watoto wadogo wa Gaza mwanzoni mwa mashambulizi ya anga ya jeshi la utawala ghasibu wa Israel huko Gaza.
Nina Hajich amesema: Mabango yanayoonyeshwa kwenye maonyesho hayo ya siku nne yatapigwa mnada mwishoni mwa maonyesho hayo na fedha zitakazopatikana kutokana na mauzo hayo zitatumika kununua misaada kwa ajili ya wakazi wa Gaza.
Amesema kuwa mashambulizi ya kinyama ya siku 22 ya Israel dhidi ya Gaza na mauaji ya raia wa eneo hilo yanafanana mno na mauaji ya kizazi yaliyofanywa na jeshi la Waserbia huko Bosnia Herzegovina katika miaka ya 1991 - 1995 na yanahesabiwa kuwa ni jinai kubwa za kivita na jinai dhidi ya binadamu. 356382