IQNA

11:13 - January 31, 2009
Habari ID: 1737906
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani:

Kuenezwa chuki dhidi ya Uislamu katika nchi za Magharibi hakuwezi kuhalalishwa

Wolfgang Schäuble, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani amekosoa siasa za kueneza chuki na woga dhidi ya Uislamu katika jamii za Magharibi na kusema kuwa jambo hilo haliwezi kuhalalishwa kwa njia yoyote ile. Schauble amesema kuwa, Waislamu wa Ujerumani wanapasa kupewa fursa ya kuabudu na kutekeleza shughuli zao za kidini bila ya kuwekewa vikwazo.

Amesema, kama wanavyofanyiwa wafuasi wa dini nyinginezo, Waislamu wanapasa kupewa haki zao zote za kidini, kisiasa, kijamii, kiuchumi na kiutamaduni katika jamii ya Ujerumani bila ya kubugudhiwa na yoyote yule.
Akizungumza kwa mnasaba wa mwaka wa 30 wa kuasisiwa Kituo cha Mazungumzo kati ya Uislamu na Ukristo cha Ujerumani katika mji wa Frankfurt, Schauble amesisitiza kuwa, fikra ya 'mgongano wa staarabu na tamaduni' ni nadharia isiyo na msingi wowote inayoenezwa na wanafikra wenye misimamo ya kupindukia mipaka katika nchi za Magharibi, misimamo ambayo haina uungaji mkono wowote katika nchi za Ulaya.
Amekumbusha kwamba, uhuru wa kusema na kujieleza, haki za wanawake, uhuru wa kuendesha shughuli za kidini na kuabudu pamoja na kunufaika wafuasi wa dini zote, na haki sawa ni miongoni mwa mambo ambayo yamebainishwa wazi katika katiba ya nchi hiyo.
Kituo cha Mazungumzo kati ya Uislamu na Ukristo cha Ujerumani kiliasisiwa katika mji wa Frankfurt mwaka 1979 kwa ajili ya kuimarisha uhusiano wa Waislamu na Wakristo, na tokea takriban miaka 10 iliyopita, Baraza la Maaskofu la Ujerumani ndilo linalosimamia shughuli za kituo hicho. Kituo hicho kinaimarisha ushirikiano wa makanisa na misikiti pamoja na jumuiya za Kiislamu za Ujerumani. Uimarishwaji wa maelewano miongoni mwa wafuasi wa dini mbili hizi za mbinguni ni miongoni mwa malengo yake makuu. 356330
captcha