IQNA

Kikao cha kumshukuru Erdogan chafanyika nchini Misri

13:29 - February 02, 2009
Habari ID: 1738759
Kikao cha kuwashukuru wanamapambano wa Kipalestina katika kukabiliana na jinai za hivi karibuni za utawala haramu wa Israel dhidi ya watu wasio na hatia katika Ukanda wa Gaza na vilevile msimamo wa hivi karibuni wa Rajab Tayyib Erdogan, Waziri Mkuu wa Uturuki dhidi ya jinai hizo, kimefanyika siku ya Jumamosi katika makao makuu ya Jumuiya ya Mawakili wa Misri huko katika mji wa Alexandria.
Katika kikao hicho ambacho kilihudhuriwa na wanawake wengi wa Misri, wanamapambano wa Harakati ya Kiislamu ya Palestina Hamas, pamoja na wakazi wa Ukanda wa Gaza walishukuriwa sana kutokana na msimamo wao wa mapambano pamoja na kusimama kidete dhidi ya jinai hizo za kinyama za Wazayuni.
Washiriki wa kikao hicho wamesisitiza juu ya umuhimu wa kupelekewa haraka misaada ya kibinadamu wakazi wa Ukanda wa Gaza wanaoteseka kutokana na kuharibiwa kila kitu walichokuwa wakikimiliki kabla ya jinai hizo za siku 22 za Wazayuni dhidi yao. Wamesema kuwa kuungwa mkono kimaada na kimaanawi wanachi hao wa Ukanda wa Gaza ni jukumu la kisheria na kiutu la kila Muislamu.
Wanawake hao wa Misri wamemshukuru sana Rajab Tayyib Erdogan Waziri Mkuu wa Uturuki, kutokana na hatua yake ya kishujaa ya kumkosoa vikali Shimon Peres, Rais wa utawala wa Kizayuni katika kikao cha Davos nchini Uswisi, na kisha kuondoka ghafla na kwa hasira katika kikao hicho kutokana na mauaji ya umati ya utawala huo dhidi ya watoto na wanawake wasio na hatia wa Ukanda wa Gaza.
Wanawake hao kwa ushirikiano wa Kamati ya Misaada ya Kibinadamu ya Misri, wameasisi Kamati ya Wanawake wa Misri kwa ajili ya Uungaji Mkono kwa Wapalestina ambapo Kauthar Abdul Fatah amechaguliwa kuwa katibu wake.
Mara tu baada ya kuchaguliwa kwake, Bi Kauthar Abdul Fatah amewataka waandishi, shakhsia wa kisiasa na kijamii na jumuiya zote za masuala ya kheri za Misri kujiunga na kamati hiyo mpya. Amesema kamati hiyo itakuwa ikiendesha shughuli zake kwa njia tofauti zikiwemo za kiutamaduni, kisheria na upashaji habari kwa manufaa ya watu wa Gaza.
Amesema, kamati hiyo pia ina lengo la kuwalea watoto ambao wamewachwa mayatima kutokana na mauaji ya umati ya utawala wa Israel dhidi ya wakazi wa Ukanda wa Gaza. 357298
captcha