Farid Jauhar al-Kalam, mtarujumi na mwandishi mashuhuri wa vitabu, anaamini kwamba tarjumi nyingi za Qur'ani zinaoonyesha wazi kwamba watarjumi wengi wa kitabu hiki kitakatifu hawazingatii sana mahitaji ya wasomaji wao katika shughuli yao hiyo.
Mtarjumi na mwandishi huyo mashuhuri amesema katika mazungumzo yake na shirika la habari la IQNA kwamba, kwa bahati mbaya idadi ya wasomaji katika kizazi hiki kipya wanaokusudiwa kunufaika na tarjuma hizo inaendelea kupungua. Ameongeza kuwa moja ya sababu zinazopeleka kupungua kwa idadi hiyo ni kutarjumiwa Qur'ani Tukufu pamoja na vitabu vingine vya kidini kwa herufi na sio kwa maana inayokusudiwa. Amesema, ni wazi kwamba tafsiri kama hizi haziwezi kukidhi mahitaji ya wasomaji wake.
Farid Jauhar al-Kalam amesema kuwa amekuwa akishuhudia kwamba lugha inayotumika katika kutarjumi Qur'ani si nyepesi inayoweza kueleweka na kila mtu. Amesema, Qur'ani ni kitabu cha muujiza cha maneno ya Mwenyezi Mungu kilichoteremshiwa Mtume Muhammad (saw), kitabu ambacho kinamuhutubu mwanadamu katika kila karne na zama.
Ameendelea kusema kuwa, kitabu hiki kimeteremshwa kwa madhumuni ya kumuongoza mwanadamu katika njia iliyonyooka na ya saada na kwa msingi huo watu wanaokitarjumu kitabu hiki kitakatifu wanapasa kuwa waangalifu na makini sana wakati wa kukifasiri huku wakizingatia mazingira na hali ya zama na nyakati zao. 384292