Salim al Hoss amesisitiza kwamba serikali ya Misri inapaswa kuacha kuivunjia heshima harakati ya mapambano na chama cha Hizbullah.
Al Hoss amesema alikuwa na matumaini kwamba serikali ya Cairo itatupilia mbali mijadala na malumbano yasiyokuwa na tija dhidi ya Hizbullah.
Amesisitiza kuwa Misri haipaswi kukuza suala la misaada ya Hizbullah kwa wananchi wa Gaza na kwamba kama kuwasaidia wananchi wa Palestina huko Gaza ni kosa la jinai, basi kadhia hiyo ni fahari kubwa na nishani ya heshima kwa harakati ya Hizbullah.
Waziri Mkuu wa zamani wa Lebanon ameongeza kuwa Misri inawajibika kuongoza umma wa Kiarabu katika kukabiliana na utawala haramu wa Israel unaotishia umma wa Kiarabu. Salim al Hoss amesema kuwa wananchi wa Misri daima wamekuwa wakiwatetea wenzao wanaokandamizwa huko Palestina na kwamba serikali ya Cairo haipaswi kushika mkondo tofauti na ule wa wananchi. 391444