Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Jumuiya ya Nchi za Kiislamu ISESCO litashiriki katika kongamano la kila mwaka la Vyombo vya Habari na Mazungumzo Kati ya Tamaduni Mbalimbali lililopangwa kufanyika tarehe 5 May nchini Tunisia.
Malengo ya kongamano hilo yametajwa kuwa ni kuchunguza njia za kutumia vyombo vya habari kwa ajili ya kujenga jamii yenye amani, kutathmini nafasi ya vyombo vya habari vya Kiislamu katika uga wa kimataifa, nafasi ya vyombo vya mawasiliano ya umma katika kusahihisha sura ya Uislamu katika nchi za Magharibi na mchango wa vyombo vya habari katika suala la mazungumzo kati ya tamaduni mbalimbali.
Mkutano huo utafanyika sambamba na kutimia miaka 27 tangu kuasisiwa shirika la ISESCO.
Shirika hilo liliasisiwa mwaka 1982 kwa lengo la kukidhi baadhi ya matakwa ya Jumuiya ya Nchi za Kiislamu OIC, kueneza maarifa na utamaduni wa Kiislamu, kuondoa mifarakano kati ya nchi za Kiislamu, kusahihisha sura iliyopotoshwa ya Uislamu katika nchi za Magharibi na kutayarisha uwanja mzuri wa maendeleo na ustawi wa nchi za Kiislamu katika nyanja mbalimbali. 397073