Akibainisha suala hilo, Gardell amesema kuwa mipango yote ya kutuma meli hiyo huko Gaza imekamilika na kwamba wabunge kutoka pambe zote za dunia akiwemo George Galloway, mbunge wa Uingereza na idadi kadhaa ya wabunge wa Sweden wataandamana na Meli hiyo kuelekea Gaza. Ameongeza kuwa meli hiyo itabeba misaada ya dharura ikiwemo ya chakula, madawa, zana za ujenzi kwa ajili ya kukarabati nyumba zilizoharibiwa na jeshi la utawala haramu katika kipindi cha siku 22 za hujuma ya kinyama dhidi ya wakazi wasio na hatia wa ukanda huo. Amesema, meli hiyo pia itabeba zana za kukarabati mabomba ya maji safi ya kunywa na kurekebisha mabomba ya maji machafu. Ameongeza kuwa, hatua hiyo imechukuliwa kwa madhumuni ya kuvunja na kulaani mzingiro wa kidhulma unaotekelezwa na utawala wa Israel dhidi ya watu wa Gaza. Huku ikikaribisha hatua hiyo, Kamati Andamizi ya Gaza imezitaka nchi zote za Ulaya na Kiarabu kupeleka misaada kama hiyo ya kibinadamu katika ukanda huo ili kuushinikiza utawala haramu wa Israel ufungue vivuko vya Ukanda wa Gaza kwa shabaha ya kuruhusu kuingizwa huko misaada zaidi ya kimataifa ya kibinadamu. 403962