Ayatullah Khamenei amezungumzia pia mwenendo wa uchaguzi wa Rais uliofanyika siku chache zilizopita hapa nchini na masuala yaliyojitokeza baada ya uchaguzi na akasema: "Mahudhurio makubwa na yasiyokuwa na kifani ya wananchi wa Iran katika uchaguzi wa Rais wa tarehe 12 Juni na kujiamini kwa taifa kubwa la Iran katika siku hiyo ilikuwa zilzala na mtetemeko mkubwa wa kisiasa kwa maadui na sherehe ya kihistoria ya wapenzi wa Iran na Mapinduzi ya Kiislamu.
Amesema kuwa wananchi wote milioni 40 waliopiga kura katika uchaguzi huo walitoa kura ya ndiyo kwa Imam Khomeini, Mapinduzi ya Kiislamu na mashahidi wote wa mapinduzi hayo na kwamba wagombea wote wanne katika uchaguzi huo ni wafuasi wa mfumo wa Kiislamu nchini Iran na kwa msingi huo wanapaswa kushughulikia masuala yao kwa kufuata sheria za nchi.
Katika hotuba ya pili ya swala ya Ijuma ya Tehran ambayo ilikatizwa mara kwa mara kwa takbira na nara za hamasa za maelfu ya wananchi waliohudhuria ibada hiyo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran alifafanua mambo mbalimbali yanayohusiana na uchaguzi wa Rais nchini Iran akilihutubu taifa la Iran, wagombea wa uchaguzi wa Rais, wasomi, wanaharakati wa kisiasa na viongozi wa baadhi ya nchi za kibeberu za Magharibi. Amewapongeza wananchi wa Iran kwa mahudhurio yao makubwa katika uchaguzi uliopita wa Rais akisema kuwa zoezi hilo lilikuwa maonyesho adhimu ya kuwajibika. Amesisitiza kuwa hamasa isiyokuwa na kifani ya tarehe 12 Juni ni tangazo la kufungamana wananchi na serikali ya Kiislamu na kwamba kushiriki kwa silimia 85 ya wapigaji kura katika zoezi hilo ni dalili ya rehema na baraka za Mola Muumba na dua za Imam wa zama Mahdi (as) kwa taifa la Iran na serikali ya Kiislamu.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa mahudhurio makubwa ya vijana katika zoezi la uchaguzi wa Rais wa Iran ni dalili ya kuendelea ari ya kisiasa ya kizazi cha kwanza cha Mapinduzi ya Kiislamu katika kizazi cha vijana wa sasa na akaongeza kuwa: "Ninatoa heshima kubwa kwa adhama ya taifa la Iran na tabaka la vijana." Ameashiria pia tofauti za kimitazamo za wananchi na kura zao kwa wagombea mbalimbali katika uchaguzi uliopita wa Rais na akasema kuwa, hisia za kuwajibika kwa ajili ya kulinda nchi na serikali ya Kiislamu ya Iran zinaoneka katika kura zote zilizopigwa na wananchi kwa wagombea tofauti. Amesema, kuhudhuria wanaume kwa wanawake, vijana kwa wazee, kaumu tofauti, wafuasi wa madhehebu mbalimbali na watu wa mijini na vijijini katika uchaguzi huo ni hamasa kubwa ambayo kamwe haitasahaulika iliyozua mtetemeko mkubwa wa kisiasa kwa maadui na kuwa sherehe halisi na ya kihistoria kwa wapenzi wa taifa la Iran kote duniani. Ayatullah Khamenei amesema kuwa mahudhurio ya watu milioni 40 katika zoezi la uchaguzi wa Rais wa tarehe 12 Juni hapa nchini ni sherehe ya kitaifa kwa ajili ya kuonyesha utiifu wa wananchi kwa hayati Imam Khomeini, Mapinduzi ya Kiislamu na mashahidi na kuongeza kuwa harakati hiyo kubwa imeupa utawala wa Kiislamu nchini Iran nguvu mpya ya kupeleka mbele gurudumu la maendeleo na ustawi na kuwadhihirishia maadui wa mfumo wa Kiislamu maana halisi ya demokrasia ya kidini.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi amesema kuwa mahudhurio makubwa ya wananchi katika zoezi la uchaguzi ambayo yaliambatana na hali ya 'kujiamini, uhuru, matarajio na utanashati' wa kitaifa ni jibu tosha kwa propaganda za kichochezi za vyombo vya habari vya mabeberu. Amesema kuwa imani ya wananchi kwa serikali ya Kiislamu ambayo ndio rasilimali kubwa zaidi ya Jamhuri ya Kiislamu, imedhihiri tena katika uchaguzi wa sasa wa Rais na sasa maadui wa Uislamu wanafanya njama za kuvuruga imani hiyo ya taifa kwa kuzusha shaka na kutilia wasiwasi uchaguzi huo na hatimaye kuzusha maswali juu ya uhalali wa mfumo wa Kiislamu wa Iran. Amesema kuwa iwapo malengo hayo maovu ya maadui yatafikiwa, itakuwa hasara kubwa ambayo haiwezi kulinganishwa na hasara nyingine yoyote.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekumbusha propaganda chafu za miezi kadhaa iliyopita zilizokuwa zikifanywa na kambi ya mabeberu wakidai kuwa kutafanyika udanganyifu katika uchaguzi wa Rais hapa nchini na akasema: "Katika hotuba yangu ya tarehe 21 Machi niliwatahadharisha marafiki hapa nchini wasikariri madai ya maadui kuhusu udanganyifu kwani wageni hao wana nia ya kuharibu imani ya wananchi kwa mfumo wa Kiislamu iliyopatikana katika kipindi chote cha miaka 30 iliyopita.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria ushindani huru na mkali wa wagombea kiti cha Rais katika kipindi cha kampeni za uchaguzi ikiwa ni pamoja na midahalo ya wazi katika televisheni na akasema: Ushindani huo ulikuwa kati ya mirengo inayoamini Mapinduzi ya Kiislamu, lakini vyombo vya habari vyenye mfungamano na Wazayuni waovu vilieneza uongo kwamba ushindani huo ni ugomvi kati ya wapinzani na waungaji mkono wa mfumo wa Kiislamu wa Iran.
Ameashiria jinsi anavyowajua vyema wagombea wanne katika kinyang'anyiro cha urais wa Iran na akasema kuwa mmoja kati yao ni Rais wa Jamhuri mwenye kuhudumia wananchi, mwenye kujituma na anayeaminika. Mwingine alikuwa Waziri Mkuu wa Iran na watatu alikuwa Kamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu na mmoja wa makamanda wakuu wakati wa vita vya kujitetea kutakatifu. Mgombea mwingine alikuwa Spika wa Bunge la Iran kwa vipindi viwili na kwa msingi huo wagombea wote hao ni watu wa serikali ya Kiislamu ya Iran na mfumo wa Kiislamu na ushindani wao ulikuwa ushindani wa watu wa ndani ya mfumo mmoja, kinyume kabisa na propaganda chafu za vyombo vya habari vyenye mfungamano na Uzayuni, Marekani na Uingereza.
Ayatullah Khamenei ameashiria pia hitilafu za kimitazamo, mielekeo ya kisiasa na sera za watu wanne waliogombea kiti cha Rais wa Iran na akasema, hitilafu hizo ni hitilafu kati ya watu wa ndani ya nyumba moja na kwamba yeye mwenyewe anawaona baadhi yao kuwa bora zaidi kuliko wengine katika kuhudumia taifa lakini hakutangaza wazi mtazamo wake kuhusu wagombea hao kwa wananchi kabla ya uchaguzi, kwani haikuwa lazima wananchi wafuate mtazamo huo, kwa sababu uchaguzi ni mali ya wananchi na matokeo yake hufuata maoni na kura za wananchi wenyewe.
Amesifu midahalo ya wagombea hao wanne katika televisheni na akasema kuwa midahalo ya wazi na ya shika nikushike ilibatilisha propaganda chafu za madola ya kigeni ambayo yalitaja kampeni za uchaguzi hapa nchini kuwa si za kweli. Ametaja uwazi na ukali wa midahalo hiyo na pia hali ya wagombea kulazimika kujitetea mbele ya wimbi la ukosoaji na kubainika wazi misimamo ya watu na makundi mbalimbali kuwa ni katika mambo mazuri ya midahalo hiyo na akaongeza kuwa, wananchi walipata uwezo mzuri wa kutoa maamuzi yao kuhusu wagombea mbalimbali kwa kushuhudia na kusikiliza midahalo hiyo na ratiba nyingine za kampeni na kuhisi kwamba serikali ya Kiislamu ya Iran haina kitu cha kuficha na inawapa wananchi haki ya kuchagua.
Ayatullah Ali Khamenei ameutaja uhuru wa kusema, kukuza uwezo wa kutafakari na kuzidisha uwezo wa kuchagua wa mwananchi kuwa ni matunda mengine mazuri ya midahalo hiyo na akasema kuwa, moja ya sababu ya kuongezeka kura milioni kumi zaidi katika uchaguzi wa sasa ikilinganishwa na chaguzi zilizopita, ni kushirikishwa kifikra wananchi katika uchaguzi wa sasa ambako kuliwavutia wananchi, kwa msingi huo, midahalo katika mtazamo huo ni jambo la kupongezwa.
Vilevile amehamasisha suala la kuendelezwa midahalo katika nyanja za uendeshaji wa masuala ya nchi na akasema kuwa, midahalo hiyo inapaswa kuendelezwa baada ya kutenganishwa na baadhi ya masuala hasi ili watu na viongozi wote waweze kukosolewa na kujitetea.
Ayatullah Ali Khamenei ameashiria baadhi ya nukta mbaya za midahalo hiyo kama kuzusha uhasama, kutegemea tetesi, udhaifu wa hoja zinazotumiwa katika baadhi ya mijadala, jazba na kupandwa na hasira pande mbili za mdahalo na akasema: "Inasikitisha kuwa baadhi ya midahalo hiyo ilichukua sura ya kuchafuana na kuharibu faili la utendaji wa serikali ya sasa na serikali zilizotangulia na hivyo kuzusha wasiwasi na mivutano miongoni mwa waungaji mkono wa wagombea hao.
Ameashiria makosa ya pande mbili zilizoshiriki katika midahalo hiyo na akasema, upande mmoja ulikuwa ukimtuhumu na kumdhalilisha Rais wa kisheria wa nchi kwa kutumia maneno ya wazi na yanayotia aibu na kutoa takwimu zisizokua sahihi kuhusu utendaji kazi wa serikali. 'Walimwita Rais aliyechaguliwa na wananchi kuwa ni mrongo, mtu anayeamini hurafa na mpiga ramli na kutupilia mbali maadili, sheria na insafu. Upande wa pili nao ulichukua hatua kama hiyo na kushusha chini utendaji mzuri wa miaka 30 ya Mapinduzi ya Kiislamu na kutilia shaka shakhsia ambao wamesabilia sehemu ya umri wao kwa ajili ya mfumo wa Kiislamu hapa nchini kwa kutaja tuhuma ambazo hazikuthibitishwa mahakamani". Amesisitiza Ayatullah Khamenei
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekosoa mjadala wa ufisadi na ubadhirifu wa mali ya umma uliohusishwa na watu wa karibu ya Sheikh Hashimi Rafsanjani na Natiq Nury na akasema kuwa, hakuna mtu aliyewatuhumu shakhsia hao kuwa ni wafisadi, lakini mtu yeyote mwenye madai dhidi ya jamaa zao hapaswi kuyatangaza katika vyombo vya habari kabla ya kuthibitishwa katika vyombo vya sheria, kwani hatua kama hizo zinasababisha utata katika jamii hususan katika fikra za kizazi cha vijana.
Ameashiria uhusiano wake wa zaidi ya miaka hamsini na Sheikh Hashimi Rafsanjani na pia huduma za shakhsia huyo kwa mapinduzi na serikali ya Kiislamu na akasema kuwa, katika kipindi cha mapambano dhidi ya utawala dhalimu wa Shah, bwana Rafsanjani alikuwa miongoni mwa watu muhimu wa harakati na baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu alikuwa mmoja kati ya watu wenye taathira kubwa waliokuwa pamoja na Imam Khomeini na alifika hata kwenye mipaka ya kuuawa shahidi kwa mara kadhaa. Amesema kwamba baada ya Imam Khomeini kuaga dunia Sheikh Rafsanjani amekuwa pamoja na uongozi wa taifa hili hadi hii leo.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa Sheikh Rafsanjani alikuwa akitoa mali yake kabla ya Mapinduzi ya Kiislamu kwa ajili ya kuendesha mapambano na katika kipindi cha miaka 30 iliyopita ameshika nyadhifa nyingi katika vipindi mbalimbali nyeti akihudumia mapinduzi na serikali ya Kiislamu na kamwe hajawahi kukusanya mali kwa ajili yake binafsi kutokana na Mapinduzi ya Kiislamu. Amesema kuwa ukweli huo unapaswa kutiliwa maanani na wananchi.
Wakati huo huo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria hitilafu za kawaida za kimitazamo kati yake na Rafsanjani kuhusu masuala mbalimbali na akasema kwamba, hitilafu hizo za kimitazamo ni jambo la kawaida na hazipaswi kutazamwa vingine na wananchi. Amesema kuwa tangu yapata miaka minne iliyopita kulikuwepo hitilafu kati ya Sheikh Rafsanjani na Rais wa Jamhuri kuhusu masuala ya kigeni, namna ya kutekeleza uadilifu wa kijamii na baadhi ya masuala ya kiutamaduni na kwamba mtazamo wa Rais unakaribiana zaidi na mtazamo wake yeye mwenyewe Kiongozi Muadhamu.
Amemtaja pia Natiq Nury kuwa ni miongoni mwa shakhsia waliotoa huduma kubwa kwa Mapinduzi ya Kiislamu na kwamba hakuna shaka yoyote katika mfungamano wake na serikali na mapinduzi hayo.
Ayatullah Khamenei amesisitiza tena juu ya udharura wa kuondolewa nakisi za midahalo na akasema kuwa baada ya midahalo hiyo alimtahadharisha Rais wa Jamhuri kwa sababu alijua vyema kwamba atachukua tahadhari hiyo.
Amesisitiza tena juu ya msimamo wa serikali wa kupambana vikali na ufisadi na ubadhirifu wa mali ya umma na akasema kuwa, kama ufisadi usingekuwepo basi miaka kadhaa iliyopita asingetuma barua yenye vipengee vinane kwa wakuu wa vyombo vikuu vitatu vya dola. Hata hivyo amesisitiza kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni miongoni mwa tawala safi zaidi za kisiasa na kijamii duniani katika upande huo na si sawa kuihusisha nchi na ufisadi kwa kutegemea vituo vya Kizayuni au kutoa tuhuma za ufisadi dhidi ya watu na viongozi bila ya ushahidi.
Akitoa tathmini ya sehemu hii ya hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa tarehe 12 Juni taifa la Iran lilionyesha hamasa ya kihistoria na kimataifa lakini baadhi ya maadui wanafanya njama za kudhihirisha ushindi huo mutlaki wa serikali ya Kiislamu kuwa ni kushindwa kitaifa na kuzuia sifa hiyo ya kushiriki kiwango kikubwa cha wananchi katika uchaguzi ili isisajiliwe katika historia kwa jina la taifa la Iran kwa kutilia shaka au kuzusha utata kuhusu uchaguzi huo. Amesisitiza kuwa njama hizo zimefeli na haiwezekani kubadilisha ukweli huo.
Ayatullah Khamenei amelihutubu taifa akisema: Watu wote waliotoa kura zao kwa mmoja kati ya wagombea wanne wa uchaguzi wa Rais wako katika kambi ya Mapinduzi ya Kiislamu na mfumo wa Kiislamu wa Iran na watapata ujira wao kutoka kwa Mola, na kwa sababu hiyo, ni lazima kusema kuwa mrengo wa Mapinduzi ya Kiislamu umepata kura milioni 40 na si kura milioni 24 zilizotolewa kwa Rais wa Jamhuri aliyechaguliwa na wananchi.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa wananchi hawana wasiwasi wowote kuhusu suala hilo lakini waungaji mkono wa wagombea pia wanapaswa kutambua kwamba serikali ya Jamhuri ya Kiislamu haiwezi kufanya hiana katika kura za wananchi. Amesisitiza kuwa muundo wa kisheria unaohusiana na uchaguzi hapa nchini hautoi mwanya wa kufanyika udanganyifu wa kawaida, seuze udanganyifu wa kura milioni 11.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa pamoja na hayo, Baraza la Kulinda Katiba limesisitizwa kushughulikia nyaraka zilizowasilishwa na wale wenye wasiwasi kuhusu matokeo ya uchaguzi na kama kutakuwepo haja ya kuhesabiwa tena masanduku ya kura kazi hiyo ifanyike kwa kuwashirikisha wawakilishi wa wagombea.
Amesema kuwa njia za kisheria ndio marejeo ya kushughulikia malalamiko yaliyotolewa na kusisitiza kwamba hatasalimu amri mbele ya uzushi usiokuwa wa kisheria kwani katika kila uchaguzi baadhi hushindwa na iwapo sheria zitakiukwa katika uchaguzi wa sasa, basi hakuna uchaguzi utakaoaminiwa au kuwa na kinga katika siku za usoni.
Ayatullah Khamenei ameashiria ukamilifu wa sheria zinazohusiana na malalamiko ya uchaguzi na akaongeza kuwa, kama ambavyo sheria imewapa wagombea haki ya kusimamia na kuwasilisha malalamiko, vilevile imeainisha njia ya kushughulikia malalamimko hayo na kwa msingi huo, kazi zote zinapaswa kufanyika kwa mujibu wa njia sahihi za kisheria.
Akiendelea na hotuba ya pili ya swala ya Ijumaa, Ayatullah Ali Khamenei amewahutubu wanasiasa, waliogombea urais na viongozi wa vyama na mirengo mbalimbali ya kisiasa akisema: Hiki ni kipindi nyeti cha kihistoria kwa nchi hii na tukitazama hali ya dunia, Mashariki ya Kati, nchi jirani na hali ya kiuchumi ya dunia tutaona kwamba Iran imo katika kipindi muhimu cha kihistoria; kwa msingi huo ni wadhifa wetu sote kuwa macho na kutofanya makosa katika kipindi hiki.
Amesisitiza kuwa wananchi wametekeleza wadhifa wao kikamilifu katika uchaguzi wa Rais na akasema kuwa wanasiasa na wale wenye ushawishi kwa baadhi ya watu katika jamii wanapaswa kuwa waangalifu mno katika maneno na mwenendo wao, kwani msimamo wowote wa kuchupa mipaka wa watu hawa utakuwa na taathira kubwa kwa wananchi na kufikia kiwango ambacho hakiwezi kudhibitiwa na wao wenyewe.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa harakati yoyote ya kuchupa mipaka huchochea harakati nyingine kama hiyo na kusisitiza kuwa iwapo wanasiasa watapuuza sheria, basi kwa kutaka au bila ya kutaka, watabeba lawama za damu, ghasia na machafuko yatakayotukia.
Ayatullah Khamenei amesema: "Ninawausia ndugu na marafiki zangu hawa wa siku nyingi kuwa na uvumilivu na kutazama mikono ya maadui na mbwa mwitu wenye njaa na wanaovizia ambao hii leo wametupilia mbali nikabu ya udiplomasia na ninawataka wasighafilike nao." Vilevile Amewataka wagombea hao kufikiria athari za kazi zao mbele ya Mwenyezi Mungu na akasema: "Ndugu zangu! Kumbukeni wasia wa mwisho ya hayati Imam Khomeini ambaye alikuwa akisema kuwa watu wote wanapaswa kuitambua sheria kuwa ndiyo muamuzi wa mwisho.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran amesema falsafa ya uchaguzi ni kutatua hitilafu zilizopo kupitia masanduku ya kupigia kura na kwamba uchaguzi unafanyika kwa ajili ya kuweka wazi ni kitu gani wanachotaka wananchi kupitia masanduku ya kupigia kura na si kuandamana mitaani. Amehoji kwamba, kama kila baada ya uchaguzi wale walioshindwa wataanzisha kambi mitaani na mkabala wake walioshinda nao wawaite wafuasi wao mitaani, basi ni kwa nini uchaguzi unafanyika? Ni dhambi gani waliyofanya wananchi ili kutokana na kazi zetu wazuiwe kufanya shughuli zao zao za kila siku?
Amesema kuwa mikusanyiko ya mitaani ni maficho bora ya magaidi na vibaraka na akaongeza kuwa iwapo kutatukia tukio lolote katika maandamano hayo ni nani atakayebeba lawama za tukio hilo? Nani atatoa jibu la mauaji ya watu wa kawaida na vijana wa kujitolea waliopoteza maisha katika siku za hivi karibuni? Nani atakayejibu na kubeba lawama za harakati yoyote ya kulipiza kisasi cha mauaji kama hayo?
Kiongozi Muadhamu amesema kwamba kutunishiana misuli mitaani ni kutia doa uchaguzi na demokrasia na akazitaka pande zote kukomesha mwenendo huo usiokuwa sahihi, la sivyo watabebeshwa lamawa za athari zake. Amesema kuwa baadhi ya watu wanapaswa kuelewa kwamba hawawezi kuishinikiza serikali kwa mijumuiko ya mitaani na wala viongozi wa serikali hawatalazimika kutekeleza matakwa yao kwa kutilia maanani maslahi ya taifa, kwani kusalimu amri mbele ya matakwa yasiyokuwa ya kisheria kutokana na mashinikizo ni mwanzo wa aina fulani ya udikteta.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa fikra na mahesabu hayo ni makosa na kama zitakuwa na athari mbaya, basi zitawakumba moja kwa moja vinara wake wanaojificha nyuma ya pazia. Amesisitiza pia kuwa kama italazimika basi wananchi watatambulishwa vinara hao katika wakati wake.
Ayatullah Khamenei ametoa wito wa kuwepo udugu, maelewano na kuheshimu sheria na akasema kuwa njia ya sheria na upendo iko wazi na ni matarajio kwamba watu wote watafuata njia hiyo na kuthamini sherehe ya ushindi wa wananchi milioni 40 waliopiga kura na kutomruhusu adui kuvuruga sherehe hiyo kubwa. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameonya kwamba iwapo baadhi ya watu watataka kufuata njia nyingine basi wakati huo ataingilia kati na kuzungumza na wananchi kwa uwazi zaidi.
Akiendelea kujadili suala la uchaguzi wa Rais nchini Iran, Ayatullah Khamenei ameashiria misimamo ya viongozi wa baadhi ya nchi za Ulaya na Marekani na akasema kuwa kabla ya kuanza uchaguzi huo vyombo vya habari vya Magharibi na viongozi wa nchi hizo walifanya njama za kutilia shaka uchaguzi wa Rais nchini Iran kwa shabaha ya kuathiri kiwango cha mahudhurio ya wananchi katika zoezi hilo, lakini mahudhurio makubwa ya watu milioni 40 katika uchaguzi huo umevifanya vyombo vya habari na viongozi wa nchi za Magharibi wapigwe na bumbuazi na kuwafahamisha kwamba, kumefunguliwa ukurasa mpya katika masuala yanayohusiana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambao hawana budi kuukubali.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amezungumzia pia baadhi ya malalamiko na masuala yaliyotokea baada ya uchaguzi wa Rais na akasema kuwa baadhi ya viongozi wa nchi za Magharibi wametumia fursa hiyo kupanda mawimbi na kubadilisha maneno yao na hatimaye sura zao zikaonekana wazi.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa mwanzoni mwa wiki, baadhi ya viongozi wa serikali na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi za Magharibi walidhihirisha uadui wao dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu, habithi zaidi ya wote ikiwa ni serikali ya Uingereza. Ameashiria kauli iliyonukuliwa kutoka kwa baadhi ya viongozi wa Marekani wakisema kuwa walikuwa wakisubiri kwa hamu siku kama hizi na kuona wananchi wa Iran wakiandamana mitaani na kusema kuwa katika upande wa pili wanaandika barua wakieleza hamu ya kuwa na uhusiano na Iran na kwamba wanaiheshimu Jamhuri ya Kiislamu. Amehoji kwamba, je ni kauli na msimamo upi za kusadiki?
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa sambamba na hayo vibaraka wa nchi hizo za kigeni ndani ya nchi wameanzisha harakati za uharibifu, kuchoma moto na kupora mali ya umma na ya wananchi na kuvuruga usalama. Amesema kuwa uharibifu huo hauna mfungamano wowote na wananchi na waungaji mkono wa wagombea katika uchaguzi uliopita wa Rais, bali unafanywa na maadui wa taifa la Iran, vibaraka wa mashirika ya kijasusi ya nchi za Magharibi na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Ayatullah Ali Khamenei amesema kuwa hali hiyo imewatia tamaa maadui na kudhani kwamba wanaweza pia kufanya mapinduzi ya mahameli nchini Iran kama ilivyofanyika katika baadhi ya nchi ndogo kwa kutumia makumi ya mamilioni ya dola za mfanyabiashara Mzayuni. Amesisitiza kuwa hata hivyo tatizo kubwa la maadui hawa majahili ni kwamba hadi sasa hawajalitambua vyema taifa la Iran.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa baya zaidi ni machungu yaliyoelezwa na viongozi wa Marekani eti kuhusu haki za binadamu na madai yao ya kuwepo hali ngumu kwa wananchi wa Iran. Amesema, swali la kuuliza ni kuwa, nchi inayotenda jinai kubwa za mauaji huko Afghanistan na Iraq na kuusaidia kifedha na kisiasa utawala dhalimu wa Kizayuni wa Israel, inaweza vipi kuzungumzia haki za binadamu?
Ayatullah Khamenei amekumbusha mauaji ya umati yaliyotekelezwa na serikali ya Wademokrati iliyokuwa ikiongozwa na Bill Clinton dhidi ya zaidi ya wafuasi 80 wa kundi la Davids na akasema kuwa, nchi iliyowachoma moto wanawake, wanaume na watoto zaidi ya thamanini wakiwa hai itafahamu vipi haki za binadamu?
Amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni mbeba bendera ya haki za binadamu na kuwatetea watu wanaodhulumiwa na haihitaji nasaha za Wamagharibi. Amesema, viongozi na wanasiasa wa nchi za Ulaya na Marekani wanapaswa kuwa na haya walau kidogo na kuachana na matendo hayo.
Katika sehemu ya mwisho ya hotuba ya pili ya swala ya Ijumaa, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alimuhutubu Imam wa zama (as) akisema: "Ewe Sayyidi wangu! Tumetekeleza wajibu wetu na kusema yaliyopaswa kusemwa na tutaendele kusema. Tumezishika nafsi na hadhi zetu ndogo mikononi na tutazisabilia katika njia ya Uislamu na Mapinduzi ya Kiislamu. Tutaendeleza njia hii kwa nguvu zote na tunaomba dua zako wewe ambaye ndiye kiongozi halisi wa mapinduzi na nchi hii."
katika hotuba ya kwanza ya swala ya Ijumaa ya Tehran, Ayatullah Ali Khamenei aliashiria nafasi ya kumkumbuka Mwenyezi Mungu na kumwamini yeye katika kuleta utulivu wa moyo kwa waumini na akasisitiza kuwa mwanadamu anapaswa kutegemea ahadi za Mola na kukimbilia kwenye kumkumbuka Mwenyezi Mungu kuomba hifadhi mkabala wa matukio mbalimbali yanayozishawishi na kuzitia nyoyo wasiwasi. Amesema, katika hali hiyo, Mwenyezi Mungu Mkarimu huteremsha utulivu katika nyoyo za waumini na kwamba utulivu huo huimarisha zaidi hatua na harakati zao.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria matukio mbalimbali ya tangu mwanzoni mwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na akasema kuwa kila moja kati ya matukio na matufani hayo lingeweza kuangamiza taifa na serikali yoyote, lakini meli hii imara inayotegemea imani na azma kubwa ya wananchi waumini haikutikisika hata kidogo katika tufani hizo, suala ambalo ni dalili ya rehema na baraza zake Mwenyezi Mungu.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa ghururi na kumsahau Mwenyezi Mungu hukomesha rehema zake na akaongeza kuwa tunapaswa kuchunga ili jazba za kisiasa na mijadala inayotokea nchini ambayo ni jambo la kawaida katika nchi yoyote huru, isije ikatusahaulisha Mwenyezi Mungu na lengo letu kuu.
Amewakumbusha vijana kuwa na imana thabiti ya Mwenyezi Mungu na akawausia wananchi wote hususan tabaka la vijana kutumia fursa zote za kiroho na kimaanawi. Amesema kuwa mwezi wa Rajab umekaribia na tunapaswa kutumia fursa hiyo kufaidika na dua za mwezi huo ambazo ni bahari ya elimu na maarifa.
422237