IQNA

16:23 - August 12, 2026
Habari ID: 3482617

Visa 231 vya Chuki dhidi ya Uislamu nchini Ujerumani katika nusu ya kwanza ya Mwaka 2026

IQNA – Katikati ya hofu inayokua kuhusu wimbi la chuki dhidi ya Uislamu (Islamophobia) nchini Ujerumani, mamlaka zimeandikisha visa 231 vya uhalifu dhidi ya Waislamu nchini humo katika nusu ya kwanza ya mwaka 2026.

c

Takwimu hizi zimetolewa na serikali kufuatia swali la kibunge lililoulizwa na wabunge kutoka Chama cha Kijani (Green Party). Serikali imesema kuwa takwimu hizi, ambazo zinajumuisha kesi zilizowekwa chini ya Chuki Dhidi ya Uislamu kama uhalifu wenye motisha ya kisiasa, ni za awali na zinaweza kurekebishwa.

Kulingana na data hizo, polisi wamewatambua washukiwa 127 katika visa hivyo, lakini hakuna aliyekamatwa kufikia sasa. Kati ya visa 231 vya uhalifu dhidi ya Waislamu, visa 33 vilitekelezwa kupitia mtandao.

Mamlaka zimeandikisha kesi 44 za uchochezi wa chuki, kesi 13 zinazohusisha alama za mashirika yasiyo ya kikatiba, visa 11 vya uhalifu wa kimabavu, visa tisa vya kulazimisha au vitisho, na kesi tatu za uharibifu wa mali. Visa vingine 47 viliainishwa kama “uhalifu mwingine.”

Ingawa idadi ya visa vilivyoandikishwa ni ya chini ikilinganishwa na mwaka uliopita—ambapo mamlaka za Ujerumani zilisajili visa 543 vya uhalifu dhidi ya Waislamu katika nusu ya pili ya mwaka 2025 na visa 489 katika nusu ya kwanza ya mwaka huo—serikali imesema takwimu za 2026 zinaweza kubadilika kutokana na ripoti zinazochelewa na marekebisho ya baadaye.

Shirika la Shirikisho la Kupambana na Ubaguzi (Federal Anti-Discrimination Agency) pia limeandikisha matukio ya chuki dhidi ya Waislamu, ambapo idadi kubwa zaidi iliripotiwa katika soko la ajira. Shirika hilo lilipokea ripoti 58 zinazohusu soko la ajira na 42 zinazohusu huduma binafsi na upatikanaji wa bidhaa. Visa vingine vya uhalifu dhidi ya Waislamu viliripotiwa katika sekta ya elimu, vyombo vya dola na idara ya mahakama, huduma za afya, na maeneo ya umma.

Matukio haya ya chuki dhidi ya Waislamu yanarekodiwa kupitia mfumo wa kuripoti wa polisi wa Ujerumani kwa uhalifu wenye motisha ya kisiasa, unaojulikana kama KPMD-PMK (Criminal Police Reporting Service in Cases of Politically Motivated Crime).

Ali Mete, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kiislamu ya Milli Gorus (IGMG), amesema kuwa takwimu hizi zinaonyesha kuwa mashambulizi dhidi ya Waislamu bado ni tatizo kubwa nchini Ujerumani.

“Visa 231 vya uhalifu vilivyoandikishwa katika nusu ya kwanza ya mwaka pekee ni vingi mno,” Mete aliliambia shirika la habari la IslamiQ. Aliongeza kuwa takwimu rasmi huenda zisionyeshe ukubwa kamili wa tatizo hilo, kwani si kila shambulio dhidi ya Waislamu huripotiwa kwa polisi au kuainishwa kama uhalifu wa aina hiyo. Pia alisisitiza kuwa ni muhimu kwa waathiriwa kuchukuliwa kwa uzito na kulindwa kikamilifu.

3498618

captcha