IQNA – Marekani inapaswa kulaani hatua ya Ufaransa ya kufunga msikiti mmoja nchini humo, hatua ambayo inaripotiwa kuchochewa na kisomo cha aya za Qur’ani Tukufu.
Baraza la Mahusiano ya Kiislamu ya Marekani (CAIR), ambalo ni shirika kubwa zaidi la haki za kiraia na utetezi wa Waislamu nchini Marekani, siku ya Jumatatu liliitaka Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani (State Department) kukemea vikali hatua hiyo ya mamlaka za Paris.
Mahakama moja nchini Ufaransa imethibitisha uamuzi wa kufungwa kwa msikiti mmoja karibu na jiji la Paris kwa muda wa miezi sita. Wakili wa haki za binadamu, Rafik Chekkat, amesema kuwa mamlaka hizo zilijenga hoja yao sehemu kwa kuzingatia madai kuwa maimamu wa msikiti huo “walinukuu… vifungu saba kutoka katika Qur’ani na kurejelea kazi kuu za utamaduni wa Kiislamu…”
Katika taarifa yake, CAIR, yenye makao makuu yake jijini Washington, D.C., ilisema:
“Hakuna serikali yoyote iliyo na haki ya kufunga kanisa, sinagogi, msikiti, au nyumba yoyote ya ibada kwa sababu tu ya kusoma maandiko kutoka katika kitabu kitakatifu cha imani yao. Kufunga msikiti kwa sababu ya kuhubiri Qur’ani Tukufu ndiyo tafsiri halisi ya ubaguzi wa kidini na dhuluma. Tunaitaka Wizara ya Mambo ya Nje, ambayo mara kwa mara imekuwa ikitoa wito wa kulindwa kwa uhuru wa kidini, kulaani uvunjaji huu wa kutisha wa uhuru unaofanywa na serikali ya Ufaransa.”
CAIR imekuwa ikilaani mara kwa mara matukio na sera za chuki dhidi ya Uislamu (Islamophobia) nchini Ufaransa.
3498607