IQNA

15:07 - August 10, 2026
Habari ID: 3482609

Qari kijana nchini Misri ana ndoto ya kuwa Abdul Basit mwingine

IQNA – Yousef, kijana kutoka Bahira nchini Misri, amewavutia wengi kwa sauti yake ya usomaji Qur’ani Tukufu na ameendeleza kipawa chake kwa kusikiliza qiraa za maqari mashuhuri kupitia mtandao. Anaota ndoto siku moja kuwa miongoni mwa majina makubwa katika uwanja wa usomaji wa Qur’ani na kufuata nyayo za Sheikh Abdul Basit Abdul Samad.

Yousef Muhammad Amr

“Nimekuwa nikihifadhi Qur’ani Tukufu tangu nilipokuwa mtoto, na ninatamani kuwa kama ustadh Abdul Basit, kwa sababu hana mfano katika fani ya usomaji wa Qur’ani,” amesema Yousef Muhammad Amr.

Alipata umaarufu kwenye mitandao ya kijamii baada ya kujaribu kuiga sauti ya Sheikh Abdul Basit Abdul Samad.

Mvuto wake haukuishia tu kwenye mitandao ya kijamii, bali uliendelea hadi hatua za awali za kipindi cha televisheni cha Misri cha vipaji vya Qur’ani kiitwacho “Dawlat Tilawah”. Mshiriki huyo kijana aliwavutia majaji na hadhira kwa sauti ya kipekee iliyogusa nyoyo kabla haijafika masikioni; sauti ambayo kwa wengi iliwarejeshea sifa halisi za madrasa ya Kimisri ya qiraa.

Yousef mdogo, ambaye kwa mapenzi anaitwa “Abdul Basit Mdogo,” ameanza kujijengea nafasi kama mmoja wa maqari wa siku zijazo. Mafanikio haya hayakuwa matokeo ya kuiga tu, bali yalitokana na uwezo wake wa pekee wa kuelewa roho ya utendaji na hisia ya unyenyekevu pamoja na heshima iliyowapambanua mashaykh wakubwa wa zamani. Watazamaji wengi wanaamini kwamba sauti yake inaashiria mustakabali wa kuwa qari mashuhuri, iwapo ataendelea kujifunza na kuimudu sanaa hii kwa ustadi zaidi.

Yousef mwenye umri wa miaka 14 anasema kuwa uhusiano wake na Qur’ani Tukufu ulianza miaka mingi iliyopita. Tayari amehifadhi juzuu ishirini za Kitabu cha Allah, na bado anaendelea na juhudi za kukamilisha hifadhi ya Qur’ani yote.

Ameongeza kuwa ustadi wake katika kusoma Qur’ani haukutokana na mafunzo rasmi ya kidini au kozi katika taasisi maalumu, bali umetokana na jitihada zake binafsi.

Alitumia saa nyingi akisikiliza faili za sauti za maqari mashuhuri kwenye mtandao, akiiga mtindo wao wa usomaji na kuchunguza kwa makini matamshi ya herufi pamoja na kanuni za tajwid, hadi sikio lake likazoea kutambua hata tofauti ndogo sana, na sauti yake ikazidi kukomaa na kustawi kwa muda.

Yousef anaeleza kuwa mama yake, kwa kuamini kipawa chake, ndiye aliyekuwa wa kwanza kumtia moyo kushiriki mashindano ya Qur’ani, yakiwemo yale ya usomaji wa kitaalamu. Wakati huohuo, baba yake ndiye aliyekuwa wa kwanza kumwelekeza kwenye uzuri wa sauti yake na kuendelea kumtia hamasa kuhifadhi na kusoma Qur’ani.

Mtoto huyu mwenye kipaji hafichi mapenzi yake makubwa kwa ustadh Abdul Basit Abdul Samad, ambaye humchukulia kuwa kigezo chake. Anaota kufuata nyayo za sheikh huyo na kuwa miongoni mwa maqari wakubwa nchini Misri na katika ulimwengu wa Kiislamu. Pia husikiliza mara kwa mara qiraa za Sheikh Muhammad Siddiq Minshawi, na huvutiwa mno na hali ya kiroho pamoja na unyenyekevu uliomo katika sauti yake.

Kwa Yousef, umaarufu alioupata kwenye mitandao ya kijamii si lengo la mwisho; bali anaona kuwa ni amana kubwa inayomsukuma kuboresha uwezo wake na kudumisha tabia njema inayomstahili msomaji wa Qur’ani. Anaamini kwa dhati kwamba kuwa na sauti nzuri pekee hakutoshi, bali ni lazima iandamane na umilisi, ikhlasi, na utendaji bora.

Yousef ana ujumbe rahisi lakini wa kina, akiwatia moyo watoto na vijana kuhifadhi Qur’ani Tukufu. Anaieleza Qur’ani kuwa ni rafiki bora wa mwanadamu, chemchemi ya baraka na ulinzi wa Mola, na njia ya mafanikio duniani na Akhera.

3498587

captcha