IQNA

Matembezi ya Arbaeen yaendeshwa kwa usalama na utaratibu wa Juu

16:21 - August 02, 2026
Habari ID: 3482575
a
IQNA – Balozi wa Iran nchini Iraq amesema kuwa Mashaya au matembezi ya Arbaeen ya mwaka huu yanaendeshwa kwa utukufu mkubwa zaidi, kwa utaratibu mzuri na ikiwa na changamoto chache ikilinganishwa na miaka iliyopita.

Akizungumza na Radio Arbaeen, Mohammad Kazem Al-Sadeq alisema: “Mwaka baada ya mwaka, Arbaeen inazidi kuwa yenye utukufu mkubwa, yenye mpangilio bora na inaendeshwa kwa matatizo machache zaidi. Katika siku zilizopita, nimetembelea njia nyingi kuu za mazuwar, zikiwemo vituo vya mpakani vya Mehran, Shalamcheh na Chazabeh, pamoja na Kadhimiya na Samarra. Kwa bahati nzuri, mazuwar wa Iran wanafanya ziara yao wakiwa katika usalama kamili na katika mazingira mazuri.”

Aliishukuru serikali na wananchi wa Iraq na kusema: “Ndugu zetu wa Iraq wamefanya juhudi kubwa zaidi ya matarajio katika kuwapokea mazuwar na kuwapatia huduma. Wanastahili shukrani zetu za dhati.”

Akisisitiza kwamba Arbaeen ya mwaka huu inaendeshwa ikiwa na changamoto chache sana, Al-Sadeq alisema: “Katika mikutano yangu na maafisa wa Iraq katika maeneo mbalimbali, nilibaini kwamba katika miaka iliyopita mazungumzo yetu mara nyingi yalijikita katika matatizo, matukio na masuala ya usalama. Lakini mwaka huu, kwa neema ya Mwenyezi Mungu, tunashuhudia Arbaeen inayofanyika kwa utulivu, usalama na mpangilio mzuri. Kwa sasa tunazungumzia zaidi mafanikio yake kuliko changamoto zake.”

Akizungumzia kuboreshwa kwa huduma katika vituo vya mpakani, aliongeza kuwa huduma hizo zimeimarika kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa na miaka iliyopita. Alisema miundombinu, njia za usafiri na huduma kwa mazuwar zimeboreshwa, huku mazuwar wanaoingia Iraq au kurejea Iran wakieleza kuridhishwa kwao na hatua zilizochukuliwa na maafisa wa pande zote mbili za mpaka.

Alieleza matumaini yake kwamba siku zilizobaki za maombolezo ya  Arbaeen zitaendelea katika amani na usalama kamili, bila matatizo yoyote.

Balozi huyo wa Iran pia alizungumzia shughuli za makao makuu ya huduma ya Iran nchini Iraq, akisema kuwa vituo 10 vya huduma vinafanya kazi katika miji ya Basra, Kadhimiya, Najaf, Karbala, Erbil na Sulaymaniyah, pamoja na katika vituo vya mpakani vya Shalamcheh, Chazabeh na Khosravi, kwa ajili ya kuwasaidia mazuwar.

Aliongeza kuwa kamati nane za kitaalamu, zikiwemo kamati za masuala ya kiutamaduni, habari, uokoaji na watu waliopotea, huduma za afya, usafirishaji na ugavi, usalama pamoja na vitengo vingine vya usaidizi, zinafanya kazi saa zote. Mazuwar wanaweza kutembelea vituo hivyo kwa ajili ya kupata mwongozo, huku changamoto zozote wanazokumbana nazo zikishughulikiwa kwa haraka iwezekanavyo.

Al-Sadeq alihitimisha kwa kuwashukuru mazuwar wa Iran kwa kusimamia safari zao kwa uwajibikaji, kushirikiana na maafisa na kuzingatia utaratibu pamoja na kanuni zilizowekwa.

3498499

captcha