IQNA

Mwakilishi wa Iran katika Mashindano ya Kimataifa ya Qur’ani Malaysia ateuliwa

7:40 - August 01, 2026
Habari ID: 3482562
m
IQNA – Mwakilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mashindano yajayo ya kimataifa ya Qur’ani Tukufu nchini Malaysia amechaguliwa rasmi.

Asghar Khosravi Sahlabadi, Mkuu wa Idara ya Mashindano katika Kituo cha Masuala ya Qur’ani cha Shirika la Awqaf na Mambo ya Hisani, ameliambia shirika la IQNA kuwa Sayyid Sadeq Moslemi ndiye atakayeiwakilisha Iran katika tukio hilo la kimataifa.

Khosravi Sahlabadi ameeleza kuwa mashindano hayo ya 66,  ambayo yanajulikana kama Mkutano wa Kimataifa wa Usomaji na Uhifadhi wa Qur’ani (MTHQA), yatafanyika nchini Malaysia kuanzia Oktoba 4 hadi 10, 2026.

Alibainisha kuwa, kwa mujibu wa tangazo la Kamati ya Kualika na Kutuma Wasomaji wa Qur’ani, Sayyid Sadeq Moslemi, ambaye ni Qari (msomaji) aliyeibuka mshindi wa pili katika Mashindano ya 48 ya Kitaifa ya Qur’ani ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, atatumwa Malaysia kwa ajili ya kushindana.

Khosravi alifafanua kuwa, kwa mujibu wa mwaliko uliotumwa kutoka Malaysia, Iran ilialikwa kutuma wawakilishi katika makundi mawili ya wanaume na wanawake katika kitengo cha Usomaji (Qira’a) wa Qur’ani.

Hata hivyo, amesema haiwezekani kutuma msomaji katika kundi la wanawake kutokana na masuala kadhaa ya kidini (kwa kuzingatia kanuni za ndani za Kiislamu). Aliongeza kuwa hakukuwa na mwaliko kwa Iran kutuma wawakilishi katika kitengo cha hifdhi.

Kwa hivyo, alifafanua, Iran itashindana pekee katika kitengo cha usomaji katika kundi la wanaume la tukio hilo la Qur’ani nchini Malaysia.

Pia, alibainisha kuwa mashindano ya Qur’ani ya Malaysia hufanyika kwa hatua mbili: mtandaoni (virtual) na ana kwa ana (in-person). Katika hatua ya mtandaoni, kila msomaji husoma kwa takribani dakika mbili, kisha baada ya kutathminiwa na majaji, wale walio bora huchaguliwa kushiriki katika hatua ya ana kwa ana.

Mwaka jana, Mkutano wa 65 wa Kimataifa wa Usomaji na Uhifadhi wa Qur’ani (MTHQA) ulifanyika katika Kituo cha Biashara cha Dunia mjini Kuala Lumpur kuanzia Agosti 2 hadi 9. Tukio hilo liliwaleta pamoja washiriki 71 kutoka nchi 49 na lilijumuisha vitengo vya qiraa na hifdhi.

3498463

Habari zinazohusiana
captcha