IQNA – Katika kile kinachothibitisha kuwa nuru ya Qur’ani Tukufu haina mipaka, Mahmoud Hassan Ashrafi, kijana mwenye umri wa miaka 18 kutoka Bangladesh ambaye ana ulemavu wa macho na hivyo haoni, anashiriki katika hatua ya fainali ya Mashindano ya 46 ya kimataifa ya Qur’ani Tukufu huko Makka, Saudia.
Hadithi ya Mahmoud ni kielelezo cha uwezo wa ajabu wa imani. Ingawa alizaliwa akiwa na ulemavu wa macho, uwezo wake wa kuhifadhi kitabu kitukufu cha Allah kwa njia ya kusikiliza qiraa mbalimbali umemwezesha kufika mbali. Akiwa na umri wa miaka saba, Mahmoud alianza safari yake ya kuhifadhi, na kwa msaada na mwongozo wa baba yake, alifanikiwa kuhifadhi Qur’ani nzima ndani ya miaka mitatu tu.
Mahmoud ni miongoni mwa washiriki 20 pekee waliochaguliwa kati ya washiriki 2,000 walioshiriki katika mchujo nchini Bangladesh. Kwa sasa, yupo Makka kushiriki kategoria ya tatu ya mashindano hayo ambayo yameandaliwa na Wizara ya Masuala ya Kiislamu, Da’wah, na Mwongozo ya Saudi Arabia.
Akizungumzia safari yake ya kwanza katika ardhi hiyo takatifu na Masjid al-Haram, Mahmoud alielezea hisia zake za shukrani na furaha, akibainisha kuwa kutembelea Mecca na kushiriki katika mashindano haya makubwa ni ndoto iliyotimia. Kwake, ulemavu wa macho haujawahi kuwa kikwazo; badala yake, ni ushahidi kuwa kwa subira na juhudi, Mwislamu anaweza kuvuka changamoto zote za kidunia.
Mashindano ya mwaka huu yana washiriki 334 kutoka nchi 133, ikiwa ni idadi kubwa zaidi kuwahi kurekodiwa. Lengo la mpango huu ni kuwahamasisha vijana wa Ummah kurejea kwenye Qur’ani kwa kuhifadhi, kufahamu, na kutafakari maana zake na kujenga ushindani unaolenga kukuza maadili ya Kiislamu.
3498591