Katika mahojiano na IQNA, Qari Hamidreza Ahmadi-Vafa amebainisha kuwa mwitikio wa mazuwaru wa Arbaeen katika vikao vya Qur'ani Tukufu wakati wa matembezi hayo umekuwa ukizidi kuimarika mwaka baada ya mwaka. Umaarufu huu mpana unaashiria kuwa idadi ya vikao na programu za Qur'ani Tukufu kando ya njia ya matembezi ya Arbaeen, hususan katika Mawakib (vituo vya huduma) makubwa, inapaswa kuongezwa, alisisitiza. Aliongeza kuwa programu za “Msafara wa Qur'ani Tukufu wa Arbaeen” zinapaswa kutilia mkazo maalum katika usomaji wa Qur'ani Tukufu. Qari Ahmadi-Vafa, msomaji mashuhuri wa kimataifa wa Iran, amekuwa sehemu ya Msafara wa Qur'ani Tukufu wa Arbaeen wa nchi hiyo mara kadhaa katika miaka ya hivi karibuni, akijihusisha moja kwa moja na shughuli za Qur'ani Tukufu katika mkusanyiko mkubwa zaidi wa watu duniani. Akitegemea uchunguzi wake wa ana kwa ana, alisisitiza fursa ya kipekee ya tukio hili kubwa katika kueneza utamaduni wa Qur'ani Tukufu na kuona kuwa kuzingatia maendeleo ya kiasi ya vikao vya usomaji ndiyo mkakati muhimu zaidi wa kuendeleza shughuli za Qur'ani Tukufu wakati wa ziara ya Arbaeen.
Alisema, “Katika nyakati ambazo nilipata fursa ya kuambatana na msafara huu, nilishuhudia wazi mwitikio mkubwa wa programu za Qur'ani Tukufu, hasa vikao vya usomaji. Mwitikio huu haujapungua, bali umekuwa mkubwa zaidi na kusambaa kila mwaka. Kwa hivyo, inatarajiwa kuwa maafisa na wahusika wataandaa mazingira ya kufanyika kwa vikao zaidi vinavyoendana na shauku hii ya umma.”
Akisisitiza hitaji la kutumia uwezo wote, fursa, na vifaa vya uenezaji ili kutambulisha na kuimarisha mzunguko wa Qur'ani Tukufu katika njia ya matembezi ya Arbaeen, alisema, “Bila shaka, katika ibada hii kuu, programu nyingine mbalimbali za kitamaduni zitafanyika, sehemu muhimu ikiwa ni fani ya nyimbo za kidini kama madahi, usomaji, na maombolezo, ambazo zina wasimamizi wake. Hivyo, inaonekana kuwa msafara wa Qur'ani Tukufu wa Arbaeen unapaswa kuelekeza utume wake mkuu katika utekelezaji wa programu za usomaji wa Qur'an'.”
Ibada ya maombolezo ya Arbaeen, ambayo mwaka huu inaangukia tarehe 4 Agosti, ni moja ya mikusanyiko mikubwa zaidi ya kidini duniani. Inaashiria siku ya 40 baada ya Ashura, kumbukumbu ya kuuawa shahidi kwa mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW), Imam Hussein (AS). Kila mwaka, umati mkubwa wa Waislamu wa madhehebu ya Shia na hata wasiokuwa Mashia, wakiwemo wafuasi wa dini nyinginezo, humiminika Karbala, ambapo kuna kaburi au Haram tukufu ya Imam Hussein (A.S), ili kutekeleza ibada za maombolezo. Mazuwaru, wengi wao wakiwa kutoka Iraq na Iran, husafiri umbali mrefu kwa miguu kuelekea mji huo mtukufu.
Iran pia hutuma msafara wa maqari na wataalamu wa Qur'an', unaojulikana kama ‘Msafara wa Noor’, nchini Iraq wakati wa matembezi ya Arbaeen. Washiriki wa Msafara wa Noor wa Iran huendesha programu mbalimbali za Qur'ani na dini, ikiwa ni pamoja na usomaji wa Qur'ani, Adhana, na Tawasheeh, barabarani katika Mashaya au matembezi ya Arbaeen kati ya Najaf na Karbala na maeneo mengine wakati wa matembezi ya Arbaeen.
3498512