IQNA

Nafasi muhimu ya Mawakib za Qur’ani katika Safari ya Arbaeen

21:47 - August 01, 2026
Habari ID: 3482570
a
IQNA – Afisa mmoja wa Iran amesisitiza umuhimu wa Mawakib za Qur’ani,vituo vya huduma vilivyojengwa kando ya njia ya Arbaeen, katika kukidhi mahitaji ya kiroho na kiutamaduni ya mahujaji.

Akizungumza na IQNA, Sayyida Maryam Mousavizadeh, Naibu Mkuu wa Bodi ya Wakurugenzi ya Muungano wa Kitaifa wa Taasisi na Mashirika ya Qur’ani na Familia, ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Muungano wa Taasisi za Qur’ani na Familia wa Mkoa wa Khuzestan, alieleza mipango ya Mawakib za Qur’ani katika mkoa huo wakati wa msimu wa Arbaeen.

Alisema ushiriki wa taasisi za umma pamoja na mipango iliyoratibiwa umewezesha kutolewa kwa huduma ambazo, mbali na kuwapatia mahujaji chakula, vinywaji na malazi, pia zinakidhi mahitaji yao ya kiutamaduni na kiroho.

Mousavizadeh alisema kuwa, pamoja na huduma za ustawi, Mawakib za Qur’ani, kwa kutegemea uwezo wa taasisi za kijamii, zinalenga kuifanya njia ya Arbaeen kuwa jukwaa la kuendeleza utamaduni wa Qur’ani na mafundisho ya Ahlul-Bayt (AS).

Aliongeza kuwa Arbaeen ni fursa ya kipekee ya kueneza utamaduni wa Qur’ani na mafundisho ya Ahlul-Bayt (AS). “Kwa msingi huo, juhudi zimefanywa kuhakikisha kwamba huduma za kiutamaduni na Qur’ani zinapewa nafasi maalumu sambamba na huduma za ustawi,” alisema.

Alisema mwaka huu, kutokana na mipango makini zaidi na usimamizi ulioratibiwa kwa ufanisi, shughuli za Mawakib za Qur’ani zitatekelezwa kwa malengo yaliyo wazi zaidi kuliko miaka iliyopita. Hivyo, mahujaji watanufaika na mazingira ya kiroho na ya Qur’ani, pamoja na huduma za kijamii.

Akizungumzia nafasi maalumu ya kituo cha mpakani cha Shalamcheh katika harakati hii ya kiutamaduni, Mousavizadeh alisema Shalamcheh ni kituo cha kwanza cha kusimama kwa wafanyaziara au mazuwari wengi wa Arbaeen wanapoelekea kwenye mazito matakatifu. Kwa hiyo, mwanzo wa safari hiyo ya kiroho unapaswa kuambatana na harufu nzuri na mwanga wa Qur’ani.

Alitaja Maukibu ya Qur’ani ya “Nur al-Hadi” mjini Khorramshahr kuwa mfano wenye mafanikio wa mtazamo huo. Alisema mbali na kuwahudumia mazuwawri, Maukibu huo umeandaa mazingira yenye utulivu na hamasa, yanayowawezesha wapenzi wa Imam Hussein (AS) kutumia muda kusoma Qur’ani, kumdhukuru Mwenyezi Mungu na kujikurubisha na Neno la Wahyi katikati ya misongamano ya wasafiri.

Mousavizadeh alisisitiza kuwa utulivu wa kiroho unaotokana na programu hizo ni tunu muhimu inayowasaidia mahujaji kuendelea na safari yao. Pia alisema jambo hilo linaonesha kuwa shughuli za Qur’ani zinaweza kuongeza kwa ufanisi ubora wa kiroho wa safari ya Arbaeen.

Arbaeen ni tukio la kidini ambalo  aghalabu huadhimishwa na Waislamu wa madhehebu Shia katika siku ya arobaini baada ya Siku ya Ashura, siku aliyouawa shahidi Imam Hussein (AS), mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW) na Imam wa tatu wa madhehebu ya Shia

Ni miongoni mwa ziara kubwa zaidi za kila mwaka duniani, ambapo mamilioni ya Waislamu wa Shia, pamoja na Wasunni wengi na wafuasi wa dini nyingine, hutembea kwa miguu kuelekea Karbala kutoka miji mbalimbali ya Iraq na nchi jirani. Mwaka huu, siku ya Arbaeen itaadhimishwa tarehe 4 Agosti.

3498488

captcha