Katika ujumbe wake, Osama al-Azhari ameeleza masikitiko makubwa na majonzi kufuatia kuaga dunia Sheikh al-Najjar, ambaye alikuwa mmoja wa wanachama wazee zaidi katika Baraza la Usomaji wa Qur’ani la Wizara ya Awqaf na mmoja wa wasomaji wakongwe zaidi katika Msikiti wa Ahmadi. Sheikh al-Najjar amefariki baada ya maisha yaliyojitolea kikamilifu katika utumishi wa Qur’ani Tukufu.
Ujumbe huo umesema kuwa marehemu Qari huyo alikuwa mwanachama mwaminifu wa wizara, ambapo alihudumu kama muadhini na msomaji wa Qur’ani katika Msikiti wa Sayyid Suwaid ulioko Manil Al-Huwayshat, na ameacha nyuma yake mfano bora wa ikhlasi, unyenyekevu, na tabia njema.
Al-Azhari amebainisha kuwa marehemu alikuwa akishiriki mara kwa mara katika vikao vya usomaji na makongamano ya Qur’ani hadi siku za mwisho za uhai wake.
Waziri wa Awqaf ametoa rambirambi zake za dhati kwa familia ya marehemu, wanafunzi wake, na marafiki zake, huku akimwomba Mwenyezi Mungu Mtukufu amjaalie rehema zake, ampe makazi mapana peponi, na amlipe ujira mwema kwa yale yote aliyoyatenda katika utumishi wa Kitabu kitukufu cha Mwenyezi Mungu, na kuiomba familia yake na ndugu zake wapewe subira na uvumilivu katika kipindi hiki cha majonzi.
Sheikh Saeed al-Najjar, mkazi wa kijiji cha Manil Al-Huwayshat katika mji wa Tanta, Mkoa wa Gharbia nchini Misri, alifariki dunia tarehe 2 Agosti akiwa na umri wa miaka 97.
Alikuwa miongoni mwa wasomaji na walimu walioshuhudia zama za dhahabu za usomaji wa Qur’ani nchini Misri, na alikuwa mwenza na msahibu wa watu mashuhuri katika nyanja hiyo, wakiwemo Sheikh Mahmoud Khalil Al-Husari na Sheikh Antar Muslim, ambao ni miongoni mwa wasomaji maarufu zaidi wa Qur’ani nchini Misri.
Maisha ya Sheikh al-Najjar katika ulingo wa Qur’ani yalihusisha miongo kadhaa ya kazi na harakati za da’wah, ambapo alihudumu kama muadhini na pia kusimamia usomaji wa Qur’ani katika Msikiti wa Sayyid Suwaid, wajibu ambao aliutimiza kwa ikhlasi na nidhamu ya hali ya juu.
Marehemu Al-Najjar alifahamika miongoni mwa wenzake na marafiki kwa shauku yake isiyokoma ya kushiriki katika vikao na mikusanyiko ya usomaji wa Qur’ani, na mchango wake katika kusimamisha maadili ya usomaji sahihi na kutukuza Kitabu cha Mwenyezi Mungu, jambo ambalo lilimfanya awe na nafasi maalum katika Wizara ya Awqaf na miongoni mwa mahudhurio ya misikitini.
Maisha yake yameshuhudia matukio mengi yaliyoonyesha utiifu wake kwa ujumbe wake wa kidini, kwani aliendelea kuwa pamoja na wanafunzi wa elimu na wapenzi wa Qur’ani hadi pumzi zake za mwisho.
3498519