Seyed Sadeq Moslemi aliiambia Shirika la Habari za Qur'ani la Kimataifa (IQNA) kwamba tangu achaguliwe kuiwakilisha Iran katika mashindano hayo yenye hadhi kubwa, ameendelea na maandalizi yake kwa kupanga ratiba ya mara kwa mara na kunufaika na mwongozo wa wataalamu pamoja na watu wenye uzoefu wa kushiriki katika mashindano hayo katika miaka iliyopita.
Akieleza sababu ya kuchaguliwa kuwa mwakilishi wa Iran, alisema kwa mujibu wa utaratibu unaotumika kwa kawaida, mshindi wa kwanza wa Mashindano ya Kitaifa ya Qur’ani ya Iran hupelekwa kushiriki katika Mashindano ya Kimataifa ya Qur’ani ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, huku mshindi wa pili akiteuliwa kushiriki katika Mashindano ya Kimataifa ya Qur’ani ya Malaysia.
“Kwa hiyo, mara tu baada ya kumalizika kwa Mashindano ya 48 ya Kitaifa ya Qur’ani, yaliyofanyika katika Mkoa wa Kurdistan mwaka uliopita, ambapo nilifanikiwa kushika nafasi ya pili katika kipengele cha usomaji, nilianza mara moja mpango madhubuti wa kudumisha na kuimarisha maandalizi yangu ya kitaaluma,” alisema.
Aliongeza: “Ilitarajiwa kwamba, kama ilivyokuwa katika awamu zilizopita, pamoja na mipango binafsi, taasisi husika zingepanga pia programu za kuwaandaa wasomaji kwa ajili ya mashindano ya Malaysia. Hata hivyo, kutokana na hali ya nchi baada ya vita vya tatu vilivyolazimishwa, baadhi ya mipango hiyo iliahirishwa au haikuweza kutekelezwa.”
Alipoulizwa iwapo kulikuwa na vikao vya maelekezo vya kumfahamisha kuhusu kanuni na taratibu za mashindano hayo, kwa kuzingatia kwamba kanuni za mashindano ya Malaysia zinatofautiana na zile za mashindano mengine ya kimataifa, alisema: “Nimekuwa nikiwasiliana na wataalamu na maprofesa wa Kamati ya Uteuzi na Usafirishaji wa Washiriki, pamoja na Kituo cha Masuala ya Qur’ani cha Shirika la Wakfu na Masuala ya Hisani. Mawasiliano hayo yamefanyika kwa kiasi kikubwa kwa njia ya mtandao, na nimefaidika kutokana na mwongozo wao pamoja na ushauri wao wa kitaaluma. Natumaini kwamba mazingira yatakapokuwa tayari, hususan katika siku za kuelekea safari, nitaweza pia kushiriki katika vikao vya maelekezo vya ana kwa ana.”
Kuhusu kunufaika na uzoefu wa wawakilishi wa Iran walioshiriki katika mashindano ya Malaysia hapo awali, alisema kutumia uzoefu wa washiriki waliotangulia ni sehemu muhimu ya mchakato wa maandalizi.
“Kwa bahati nzuri, katika mikutano ya pamoja niliyokuwa nayo na Mohsen Ghassemi, ambaye alikuwa mwakilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mashindano ya Malaysia mwaka uliopita, nilipata taarifa muhimu kuhusu mazingira ya mashindano, namna yanavyoendeshwa na mambo yanayopaswa kuzingatiwa wakati wa kushiriki,” alisema.
Aliongeza: “Vilevile, kupitia mazungumzo ya kina na Seyed Mostafa Hosseini, msomaji bora katika Mashindano ya Kimataifa ya Qur’ani ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na mwakilishi wa Iran katika awamu zilizopita za mashindano ya Malaysia, nimefaidika kutokana na nasaha muhimu pamoja na maelekezo ya kitaaluma kuhusu usomaji wa Qur’ani.”
Mashindano hayo ya Malayasia ni ya 66 mwaka huu na ni maarufu kama Mkutano wa Kimataifa wa Usomaji na Uhifadhi wa Qur’ani, kwa kifupi kama MTHQA na yamepangwa kufanyika katika hatua mbili: kwa njia ya mtandao na ana kwa ana. Hatua ya ana kwa ana ya mashindano hayo itafanyika mjini Kuala Lumpur kuanzia Oktoba 4 hadi 10, 2026.
Mwaka uliopita, tukio hilo la Qur’ani liliwakutanisha washiriki 71 kutoka nchi 49 na lilijumuisha vipengele vya kusoma na kuhifadhi Qur'ani Tukufu.
3498497