IQNA

Idadi ya mazuwar  wa Arbaeen wanaoingia Iraq yakaribia milioni 3

7:26 - August 01, 2026
Habari ID: 3482559
A
IQNA – Makao Makuu ya Usimamizi wa Ziara ya Arbaeen nchini Iraq yalitangaza siku ya Alhamisi kuwa idadi ya mazuwar au wafanyaziara wa kigeni walioingia nchini humo inakaribia kufikia milioni tatu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na makao hayo makuu, mazuwar wa kigeni 2,887,305 wamewasili Iraq hadi sasa kwa ajili ya msafara wa Arbaeen.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa utekelezaji wa mpango wa kiusalama na huduma kwa ajili ya ziara ya Arbaeen unaendelea kwa uratibu na taasisi zote za usalama, huduma na msaada. Lengo ni kuhakikisha usalama wa mahujaji wanaoingia Iraq, pamoja na kuwezesha mtiririko salama na wenye ufanisi katika vivuko vya mipakani na barabara kuu.

Hatua hizi, kwa mujibu wa taarifa hiyo, zinatekelezwa kwa uungaji mkono wa moja kwa moja wa Waziri Mkuu wa Iraq, ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu wa vikosi vya nchi hiyo.

Kwa takwimu za karibuni zilizosasishwa, kuanzia siku ya kwanza ya mwezi wa Muharram hadi mwisho wa Jumatano usiku, jumla ya mazuwar 2,887,305 waliingia Iraq. Makao Makuu hayo yaliongeza kuwa ujio wa mahujaji kutoka nchi mbalimbali kwa ajili ya kushiriki katika maadhimisho ya Arbaeen unaendelea.

Aidha, taasisi hiyo ilisisitiza kuwa vitengo vya usalama na taasisi za msaada vinaendelea na majukumu yao uwanjani kwa mujibu wa mipango iliyowekwa mapema, chini ya usimamizi wa Kamati Kuu ya Ziara za Mamilioni ya Waumini.

Arbaeen ni tukio la kidini linaloadhimishwa na Waislamu wa Kishia siku ya arobaini baada ya Siku ya Ashura, kwa kumbukumbu ya kuuawa shahidi Imam Hussein (AS), mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW) na Imam wa tatu wa Madhehebu ya Shia.

Ni miongoni mwa ziara kubwa zaidi za kila mwaka duniani, ambapo mamilioni ya Waislamu wa Kishia, pamoja na idadi kubwa ya Waislamu wa Kisunni na wafuasi wa dini nyingine, hutembea kwa miguu kuelekea Karbala kutoka miji mbalimbali ya Iraq na mataifa mengine.

3498472

Habari zinazohusiana
captcha