IQNA

Maulamaa Iran walaani kitendo cha kuichoma moto Qurani

7:56 - September 14, 2010
Habari ID: 1993203
Maulama wa ngazi za juu wa dini, viongozi wa kisiasa, jumuiya na taasisi mbalimbali katika Jamuri ya Kiislamu ya Iran zimetoa taarifa mbalimbali zikilaani vitendo vya kuchomwa moto na kuraruriwa Qur'ani Tukufu nchini Marekani.
Ayatullah Makarim Shirazi ametoa taarifa akilaani kitendo hicho kiovu na kusema inastaajabisha kuona vitendo kama hivyo vya kihayawani vikitendeka katika zama zinazodaiwa ni za kustaarabika na kuvunjia heshima kitabu cha Waislamu bilioni moja na nusu. Amesisitiza kuwa maadui wa Qur'ani wanapaswa kuelewa kwamba vitendo hivyo viovu havipunguzi lolote katika adhama na utukufu wa Qur'ani bali vinadhihirisha ukatili na unyama wao.
Ayatullah Nuri Hamedani ambaye ni miongoni mwa wanazuoni wakubwa hapa nchini pia amelaani vikali kuchomwa moto Qur'ani nchini Marekani na kusisitiza kuwa ulimwengu wa kibeberu unapaswa kujitayarisha kwa matokeo ya hasira kali za Waislamu kote duniani.
Miji mbalimbali ya Iran pia imeshuhudia maandamano makubwa ya kulaani uhalifu wa kuchomwa moto Qur'ani huko Marekani katika kumbukumbu ya matukio ya Septemba 11. Mjini Tehran maelfu ya watu wameandamana leo mbele ya ubalozi wa Uswisi unaolinda maslahi ya Marekani hapa nchini na kuchoma moto bendera za nchi hiyo. Taarifa iliyotolewa na waandamanaji hao imesisitiza kuwa tukio la kuchomwa moto Qur'ani nchini Marekani litaleta mabadiliko makubwa katika ulimwengu wa Kiislamu na kuwaamsha Waislamu wengi waliolala.
654070
captcha