Hayo yamesemwa na imamu wa Kituo cha Mahfal Zainab nchini Ufaransa Mussa Abdul Muumin katika mazungumzo yake na IQNA. Amesema inasikitisha kuona watu wanaodai kuwa wanafuata dini ya tauhidi na kumpwekesha Mwenyezi Mungu wakichoma moto Qur'ani Tukufu. Amesema kwa kutilia maanani kwamba jina la Nabii Issa Masih na Bibi Maryam (as) limetajwa mara nyingi zaidi ya jina la Nabii Muhammad (saw) katika Qur'ani, hapana shaka kuwa kitendo cha kukivunjia heshima kitabu hicho cha Mwenyezi Mungu na kukichoma moto kilichofanywa na Wakristo wenye misimamo ya kufurutu mipaka ni kumvunjia heshima kwanza Nabii Issa au Yesu Kristo.
Imam Abdul Muumin amesema watu aliopanga njama ya kuchoma moto Qur'ani tukufu na kutekeleza njama hiyo hawakufikiria vyema kabla ya kuchukua hatua hiyo kwani inawezekana vipi kwa mtu anayedai kuwa ni mfuasi wa dini ya Nabii Issa ambayo inampwekesha Mwenyezi Mungu kukichoma moto kitabu cha dini nyingine inayompwekesha na kumtakasa Mwenyezi Mungu? Amesisitiza kuwa watu waliochoma moto Qur'ani si wafuasi wa mafundisho ya Kikristo bali wana majina ya Kikristo tu.
Imam wa Kituo cha Mahfal Zainab nchini Ufaransa pia ameashiria mjadala unaotokota kuhusu suala la ujenzi wa msikiti na kituo cha Kiislamu mjini New York Marekani na akasema: "Mimi kama Muislamu ninaamini kwamba ni haki ya Waislamu kujenga msikiti katika eneo hilo." 658779