Mahmoud Hamdi Zaqzouq, Waziri wa Wakfu na Masuala ya Kiislamu wa Misri amesisitiza kuwa watu wa Misri, bila kujali madhehebu zao za kidini, wanawapenda Ahlul Beit (as) au kwa ibara nyingine Watu wa Nyumba ya Mtume (saw).
Kwa mujibu wa tovuti ya Iraqgreen.net, Zaqzouq aliyasema hayo hivi karibuni alipokutana na kuzungumza na ujumbe wa kidini wa Iraq mjini Cairo na kuongeza kuwa mjadala kuhusu makundi ya kidini huzusha mivutano na fitina kwenye jamii. Amesema, wanazuoni wa kidini wanapasa kutekeleza vyema majukumu yao katika jamii ya kuwaunganisha Waislamu na kupambana na misimamo ya kupindukia mipaka kwa manufaa ya ulimwengu mzima wa Kiislamu. Amesema wizara yake hivi karibuni imechapisha ensaiklopidia ambayo inakusanya masuala ya kifiqhi ya madhehebu tofauti ya Kiislamu.
Waziri Zaqzouq amesisitiza juu ya udharura wa kuimarisha utamaduni wa kuishi pamoja kwa amani wafuasi wa dini tofauti. Amesema, Uislamu unakubali mitazamo tofauti na kwamba unalichukulia jambo hilo kuwa linaloimarisha fikra na ukamilifu wa mwanadamu.
Mwishoni Zaqzouq ameelezea matumaini yake kwamba Iraq itafanikiwa kufikia malengo yake ya ustawi na maendeleo ambayo yatakaipelekea kuwa na athari muhimu katika Ulimwengu wa Kiislamu. 661553