Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, Jumuiya ya Wanachuo wa Ulimwengu wa Kiislamu imetoa taarifa na kumshukuru Sheikh Ahmad Tayyeb kwa kusimama kidete mbele ya matakwa haramu ya watu wenye misimamo mikali na wanaozusha mifarakano katika umma wa Kiislamu.
Jumuiya hiyo imesema umoja wa Kiislamu ni jambo la kimsingi na kwamba Mwenyezi Mungu SWT katika Qur'ani Tukufu ametoa wito kwa Waislamu wote kuungana. Jumuiya hiyo imesema umoja wa Waislamu ni muhimu katika kukabiliana na njama za maadui.
Taarifa hiyo imesema kuwa: "Hotuba na hatua za kuleta umoja za maulama wa Kiislamu kama vile misimamo ya Ayatullah Ali Khamenei na mitazamo ya Sheikh ul Azhar ni mambo yatakayoimarisha Umoja wa Kiislamu na kuondoa hitilafu na hayo ni kwa maslahi ya umma wote wa Kiislamu. Kwa hivyo Maulamaa wote wanatakiwa kuhimiza umoja wa Kiislamu na kuepusha kukurufishana na wafahamu kuwa maadui watatumia mbinu zote kuvuruga umoja wa Kiislamu ambao ndio nguzo ya nguvu za Waislamu dhidi yao".
Hivi karibuni Sheikh wa Chuo Kikuu cha al Azhar cha Misri alipinga hatua ya baadhi ya kanali za televisheni za satalaiti ya kuwakufurisha Waislamu wa madhehebu ya Shia akisema kuwa hitilafu kati ya Shia na Suni zinazushwa kwa lengo la kutumiwa katika masuala ya kisiasa. Sheikh Ahmad al Tayyib alisema kuwa wajibu wa Chuo Kikuu cha al Azhar katika awamu ya kwanza ni kuimarisha umoja wa Kiislamu na kuwakutanisha Waislamu wote katika mtazamo mmoja licha ya kuwepo hitilafu za kimitazamo na kiijtihadi.
677870