IQNA

Iran na Qatar kupambana na chuki dhidi ya Uislamu

16:46 - January 24, 2011
Habari ID: 2069745
Waziri wa Utamaduni na Muongozo wa Kiislamu wa Iran na mwenzake wa Qatar wamesisitiza kuhusu ulazima wa kuwepo ushirikiano ili kukabiliana na chuki dhidi ya Uislamu.
Waziri wa Utamaduni na Muongozo wa Kiislamu wa Iran Sayyid Muhammad Husseini amefanya mazungumzo na mwenzake wa Qatar Hamad Bin Abdulaziz Al Kuwari aliyekuwa safarini mjini Tehran.
Akiashiria uhusiano wa kirafiki wa nchi hizo mbili Husseini amesema kuwa Rais wa Iran Mahmoud Ahmadinejad na Amir wa Qatar Hamad Bin Khalifa Al Thani wameshatembeleana mara kadhaa katika miaka ya hivi karibuni jambo ambalo linaashiria uhusiano mpana wa kisiasa, kiutamaduni na kiuchumi baina ya nchi hizi mbili.
Kwingineko katika matamshi yake, Husseini ameashiria nafasi muhimu ya kanali ya televisheni ya Al Jazeera yenye makao yake mjini Doha na kuongeza kuwa kanali hiyo inaweza kushirikiana na televisheni za Iran na hivyo kuwa na nafasi kubwa katika kuarifisha Uislamu duniani na kupambana na chuki dhidi ya Uislamu.
Kwa upande wake Al Kuwari amesisitiza kuhusu umuhimu wa uhusiano wa nchi mbili na amemualika mwenzake wa Iran kutembelea Maonyesho ya Vitabu ya Dunia yatakayofanyika Qatar hivi karibuni. Amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina nafasi muhimu katika kuimarisha umoja miongoni mwa Waislamu. Vilevile amesisitiza kuhusu umuhimu wa ushirikiano wa maulamaa na wanazuoni wa Kiislamu wa Iran na Qatar.
734968



captcha