Idara ya Polisi ya McKinney imethibitisha kuwa imeongeza ulinzi karibu na Kituo cha Sufaraa na inaendelea kuwasiliana na viongozi wa kituo hicho.
Msemaji wa idara hiyo alisema kuwa hatua hiyo ni sehemu ya juhudi pana za kuhakikisha usalama wa wakazi wote wa McKinney, bila kujali dini, rangi au imani.
Kwa mujibu wa tawi la Texas la Baraza la Mahusiano ya Kiislamu Marekani (CAIR), mwanamume mmoja aligonga kengele ya Kituo cha Sufaraa mara kadhaa kabla ya kuingia ndani bila ruhusa. Kikundi hicho kilisema kuwa alitamka kwa sauti, “hapapaswi kuwa na misikiti Marekani,” pamoja na kauli nyingine za chuki.
Kituo cha Sufaraa si msikiti tu, bali ni taasisi inayotoa programu za elimu na matukio yanayohusiana na Uislamu.
CAIR ilihusisha tukio hilo na matamshi ya uchochezi yanayodaiwa kutolewa na Gavana wa Texas, Greg Abbott. Katika tamko lake, Mkurugenzi wa CAIR wa eneo la Dallas-Fort Worth, Mustafaa Carroll, alisema matukio ya chuki kama hayo yanachochewa na “kauli na sera nyingi za chuki dhidi ya Uislamu kutoka kwa Gavana Abbott na maafisa wengine wa serikali ya jimbo.”
Ripoti hii inakuja muda mfupi baada ya Abbott kusaini Mswada wa Sheria Namba 4211 katika Kaunti ya Collin, hatua iliyolenga mradi wa maendeleo wa Kituo cha Kiislamu cha East Plano, ujulikanao kama EPIC City. Wakati wa hafla ya kusaini, Abbott alirejelea mara kwa mara kile alichokiita “makazi ya Sharia,” akidai kuwa sheria hiyo inazuia jamii za kidini kuanzisha “maeneo yasiyofikika” na kuhakikisha migogoro ya ardhi inatatuliwa kwa mujibu wa sheria za Texas.
Viongozi wa EPIC wanasema kuwa mradi huo umelengwa kwa upendeleo wa kidini. Maendeleo hayo yamekumbwa na uchunguzi kadhaa, ikiwemo uchunguzi wa shirikisho uliokamilika mapema mwaka huu, na uchunguzi wa makazi wa ngazi ya jimbo ambao bado unaendelea.
CAIR imetoa wito wa kuwajibika, ikionya kuwa matamshi kama hayo yanachangia uhasama dhidi ya jamii za Kiislamu kote Texas.
3494666