IQNA

Khatibu wa Al-Aqsa akamatwa baada ya hotuba kali dhidi ya Ukimya wa Waarabu na Waislamu

18:41 - September 20, 2025
Habari ID: 3481258
IQNA – Polisi wa utawala wa Israel wamemkamata Sheikh Mohammad Sarandah, khatibu wa Msikiti wa Al-Aqsa, muda mfupi baada ya kutoa hotuba ya Ijumaa, kwa mujibu wa Waqfu wa Kiislamu wa al-Quds.

Sheikh Sarandah aliachiliwa baadaye siku hiyo hiyo, lakini akapigwa marufuku ya kuingia msikitini kwa muda wa wiki moja. Waqfu ulisema kuwa marufuku hiyo inaweza kuongezwa, ingawa haukutoa sababu rasmi.

Kukamatwa kwake kulifuatia mkusanyiko wa maelfu ya waumini waliokusanyika kwa sala ya Ijumaa katika Msikiti wa Al-Aqsa. Idara ya Waqfu wa Kiislamu ilikadiria kuwa takriban waumini 40,000 walihudhuria, licha ya vizuizi vya kiusalama vilivyowekwa na Israel, ikiwemo kufungwa kwa kivuko cha kambi ya wakimbizi ya Shuafat, ukaguzi mkali katika vituo vya kuingia mji wa kale wa al-Quds, na kuwekwa vizuizi vya chuma. Mashuhuda walisema polisi walikamata vijana na kupekua vitambulisho vya waumini.

Mamlaka za Israel hazikutoa tamko rasmi kuhusu kukamatwa kwa khatibu huyo. Khatibu wa Al-Aqsa mara kwa mara hukumbwa na vikwazo wanapozungumzia mauaji ya halaiki yanayoendelea Gaza, ambako zaidi ya Wapalestina 65,000 wameuawa tangu kuanza kwa vita mwezi Oktoba 2023.

Katika hotuba yake, Sheikh Sarandah alitoa ukosoaji mkali kwa viongozi wa mataifa ya Kiarabu na Kiislamu kuhusu msimamo wao juu ya vita hiyo. Alisema kuwa wakati watu wa Gaza wanateseka na vita, ukimya wa mataifa jirani unawaacha bila msaada.

Akitumia tamathali ya semi, alionya: “Ukimuona ndugu yako akiliwa na mbwa mwitu, fahamu kuwa muda si mrefu na wewe utakuwa mfuatayo… Moto ukiteketeza chumba kimoja cha nyumba, chumba kingine hakitasalimika,” kwa mujibu wa Shirika la Habari la Yemen (SABA).

/3494664

Habari zinazohusiana
Kishikizo: al aqsa mhubiri israel
captcha