Pezeshkian ametoa kauli hiyo siku ya Jumatatu katika ufunguzi wa Mkutano wa 39 wa Umoja wa Kiislamu Duniani unaofanyika Tehran, mkutano ambao umeleta pamoja zaidi ya wajumbe 210 kutoka ulimwengu mzima wa Kiislamu, wakiwemo mawaziri, ma-mufti wakuu, na washauri waandamizi.
Mkutano huo wa siku tano unajumuisha mijadala, uzinduzi wa vitabu, na warsha zaidi ya 200 za kimataifa.
“Iwapo ummah wa Kiislamu utaungana katika Mhimili wa Mtume (SAW), hakuna adui atakayethubutu kuvamia haki zake,” alisema Pezeshkian katika hotuba yake ya ufunguzi. Alionya kuwa “migawanyiko ya ndani imefungua milango ya dhulma na mauaji ya halaiki dhidi ya Waislamu.”
Rais huyo alitaja aya za Qur’ani na mfano wa Mtume Muhammad (SAW) alipoyapatanisha makabila yaliyokuwa yakipigana huko Madina, akisisitiza kuwa udugu ni lazima utekelezwe kwa vitendo, si kwa maneno tu. “Mtume alitangaza, ‘Waumini ni ndugu’ na huo ulikuwa mwanzo wa mafanikio yake.”
Alieleza wazi uhusiano kati ya kutokuwepo kwa umoja na uingiliaji wa mataifa ya kigeni. “Kama jamii ya Kiislamu ingekuwa na mshikamano, Marekani, Israel au taifa lolote lisingethubutu kuwashambulia Waislamu na kupuuza haki zao,” alisema. “Tatizo letu ni mgawanyiko wa ndani, na lazima tuanze na nafsi zetu.”
Rais Pezeshkian amekosoa vikali madai ya Magharibi kuhusu haki za binadamu, akisema, “Ikifanyika jambo katika jamii za Kiislamu, wao husema haki za binadamu zimekiukwa. Haki gani hizo? Zile zisizowahurumia watoto, wanawake, wazee na wagonjwa, na zinazofanya mauaji ya halaiki?”
Alikumbusha pia msimamo wa Imam Hussein (AS) huko Karbala: “Ikiwa huamini dini wala huogopi Akhera, basi angalau uwe huru dhidi ya dhulma na kiburi.” Alisema Waislamu wenyewe wanawajibika kwa kuruhusu wageni kutumia migogoro yao.
“Wao huchochea vita, huuza silaha, kuchukua mafuta yetu, na kutufanya tuendelee kugombana wenyewe,” alisema.
“Sisi ni ndugu na Wapalestina, Wairaqi, Waqatari, Waemirati, na Waislamu wote. Udugu huu lazima uwe wa kweli na wa vitendo, si kauli tu,” aliongeza.
3494522