Akizungumza na IQNA pembezoni mwa Mkutano wa 39 wa Umoja wa Kiislamu Duniani, Zuhri Yuhyi alitoa wito wa mshikamano imara miongoni mwa mataifa ya Kiislamu na akasisitiza umuhimu wa kuunga mkono Gaza kwa nguvu zaidi.
“Kwa hakika, kile tunachopaswa kufanya kama Ummah wa Kiislamu ni kushirikiana,” alisema Zuhri, ambaye ni mkuu wa Idara ya Mikakati na Fedha ya Baraza la Ushauri la Mashirika ya Kiislamu Malaysia (MAPIM).
Alisisitiza kuwa Waislamu wanapaswa kuangazia imani zao za pamoja badala ya tofauti zao, akiongeza kuwa shahada, yaani tamko la Imani la Kiislamu, inapaswa kuwa msingi wa umoja.
Zuhri alieleza kuwa kusisitiza misingi ya pamoja kunaweza kuziba ufa wa mgawanyiko ndani ya Ummah. Alisema mikusanyiko ya wanazuoni kutoka madhehebu tofauti husaidia kujenga imani na uelewano, na kwa kuwa wanazuoni huathiri jamii, mikutano kama hiyo inaweza kuyakaribisha mataifa ya Kiislamu zaidi.
Kuhusu msimamo wa Malaysia dhidi ya mauaji ya kimbari yanayoendelea Gaza, Zuhri alieleza kuwa nchi yake imekuwa ikijihusisha kwa muda mrefu na kazi za kibinadamu. Alisema wamekuwa wakitoa msaada wa chakula, mavazi ya msimu wa baridi, na shule za muda kwa Wapalestina. Kwa sasa, Wamalaysia 45 wako ndani ya msafara wa kimataifa wa misaada kwa Gaza, unaojumuisha meli 20 kutoka bandari za Hispania, Tunisia, Italia na Sicily.
Aliongeza kuwa Wamalaysia huandaa maandamano ya kila wiki nje ya ofisi ya Umoja wa Mataifa mjini Kuala Lumpur. “Ummah wa Kiislamu una wajibu wa kuilinda Msikiti wa Al-Aqsa. Ummah haujakamilika bila Al-Aqsa,” alisema.
Akinukuu maneno ya Mtume Muhammad (SAW), Zuhri alisema: “Kiungo kimoja cha mwili kinapoumia, mwili mzima huhisi maumivu. Kwa hivyo, ni lazima tuhisi uchungu wa akina baba, mama na watoto wa Gaza.”
Kauli hizi zinakuja wakati ambapo tangu kuanza kwa vita Gaza mwezi Oktoba 2023, zaidi ya Wapalestina 65,000 wameuawa katika mashambulizi ya Israel. Kamati ya Umoja wa Mataifa wiki iliyopita ilitambua vita hivyo kuwa ni mauaji ya halaiki, huku utawala wa Israel ukiendeleza mashambulizi ya ardhini na anga bila kukoma, sambamba na kuzuia misaada kuingia ukanda huo. Mashirika ya haki za binadamu yameeleza kuwa utawala huo unatumia njaa kama silaha ya vita.
Mafundisho ya Mtume na Changamoto za Kiutamaduni
Alipoulizwa kuhusu namna ya kukabiliana na athari hasi za kitamaduni, Zuhri alisema tatizo linatokana na shinikizo kutoka Magharibi na udhaifu wa ndani.
Alionya kuwa kuna juhudi za kuwatenganisha Waislamu na Qur’ani, akisema: “Wazungu wa Anglo-Saxon daima wamekuwa na ajenda ya kuiondoa Qur’ani ndani ya Ummah kwa sababu ndiyo chanzo cha nguvu zetu katika maisha.”
Alisisitiza kuwa wanazuoni wanapaswa kuchukua nafasi kubwa zaidi katika kuwaongoza vijana, akibainisha kuwa “jukumu la wanazuoni ni kuzungumza na vijana kwa lugha yao.”
Ujasiri wa Iran Wavutia
Katika sehemu nyingine ya mazungumzo yake, mwanaharakati huyo alisifu hatua ya kujilinda ya Iran katika vita vya siku 12 vilivyoanzishwa na utawala wa Israel na Marekani mwezi Juni.
Alisema nguvu iliyodhihirishwa na Iran ilikuwa “ya kushangaza na ya kuhamasisha,” na akaeleza kuwa Wamalaysia wengi wanaamini Iran ina uwezo wa kuikabili Israel.
Aliyataja mashambulizi ya Iran kuwa ni haki ya kujilinda, huku akilaani Israel kwa kuvunja kanuni za kimataifa.
Utawala wa Israel ulianzisha mashambulizi makubwa dhidi ya ardhi ya Iran tarehe 13 Juni, ukilenga maeneo ya kijeshi na ya nyuklia, na kuwaua makamanda wa juu wa kijeshi, wanasayansi wa nyuklia, pamoja na raia wa kawaida. Marekani pia ilishiriki mashambulizi hayo kwa kulenga vituo vya nyuklia vya amani katikati mwa Iran.
Jeshi la Iran, kwa kujibu, lilipiga miundombinu ya kijeshi na viwanda vya utawala huo kwa makombora ya kizazi kipya yaliyolenga kwa usahihi. Iran pia iliIjibu Marekani kwa kulenga kituo chake kikuu cha anga kilichopo Qatar.
Baada ya siku 12, utawala wa Israel ulilazimika kutangaza kusitisha mashambulizi kwa upande mmoja, kufuatia pendekezo la makubaliano kutoka Washington.
3494668