Mkutano wa kimataifa wa 'Najaf, Mji Mkuu wa Ulimwengu wa Kiislamu katika mwaka 2012' umefunguliwa rasmi katika mji huo mtakatifu kwa kuhudhuriwa na wanazuoni na watafiti mashuhuri wa Kiislamu kutoka nchi tofauti za Kiislamu na za Ulaya.
Akizungumzia suala hilo, Swalah al-Ubeidi, mmoja wa wanachama wa kamati inayoandaa mkutano huo amesema kwamba, mkutano huo umeandaliwa kufuatia kuchaguliwa mji mtakatifu wa Najaf kuwa mji mkuu wa kiutamaduni wa ulimwengu wa Kiislamu katika mwaka ujao wa 2012.
Mkutano huo unaowashirikisha watafiti mashuhuri 76 kutoka nchi 18 za dunia utadumu kwa muda wa siku tatu tokea jana Jumanne, ambapo washiriki pia watapata fursa ya kuyatembelea maeneo ya kihistoria katika mji huo na mji mwingine mtakatifu wa kufa. Amesema lengo jingine la kufanyika mkutano huo ni kuiarifisha zaidi miji miwili hiyo mitakatifu, kubainishwa nafasi ya kisiasa na kihistoria ya miji hiyo, athari zake katika siku zijazo na kuandaliwa mazingira ya kufanyika sherehe kubwa ya kuchaguliwa mji wa Najaf kuwa mji mkuu wa kiutamaduni wa Ulimwengu wa Kiislamu mwaka ujao wa 2012. Akizungumza na vyombo vya habari katika mkutano huo, Yishar Shariff mmoja wa wanazuoni mashuhuri wa Ugiriki amesema kuwa mkutano huo una nafasi muhimu katika kuimarisha ushirikiano wa wanazuoni na wasomi wa Kiislamu. Ameongeza kuwa hata kama matokea ya mkutano huo huenda yasidhihirike mara moja lakini bila shaka yatakuwa na athari kubwa ya kuwaunganisha Waislamu kutokana na kuwa wanazuoni kutoka madhehebu yote ya Kiislamu kutoka pembe tofauti za duniani wanashiriki katika kikao hicho. 760135