Akihutubia mbele ya mjumuiko mkubwa wa wananchi wa mkoa wa Kermanshah magharibi mwa Iran, Rais Ahmadinejad ameongeza kuwa, madai ya kuundwa serikali mbili katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu, ni njama za kuuokoa utawala wa Kizayuni wa Israel na kusambaratisha muqawamah wa wananchi wa Palestina. Ameongeza kuwa, nchi za Magharibi zinafanya juhudi za kuuokoa utawala ghasibu wa Kizayuni unaokaribia kusambaratika, sambamba na kuisafisha sura inayochukiza ya Marekani. Dakta Ahmadinejad ameongeza kuwa, nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani zinafanya njama za kuanzisha vita kati ya Mashia na Masuni pamoja na kuzusha ugomvi kati ya taifa la Iran na Waarabu, ili kuunusuru utawala wa Kizayuni wa Israel.
Ameongeza kuwa hila na hadaa za nchi hizo za Magharibi ni tata mno, hivyo wananchi wa eneo la Mashariki ya Kati wanapaswa kuwa macho katika kukabiliana na njama hizo.
Wakati huo huo Rais Ahmadinejad ameukosoa vikali ujumbe wa Rais Barack Obama kwa mnasaba wa siku kuu ya Nouruz na kuutaja ujumbe huo kuwa ‘tusi' kwa taifa la Iran.
Amesema kuwa Obama hakufahamu thamani za sherehe za Nowruz ambazo zinatambuliwa kimataifa. Rais Ahmadinejad amesema siku kuu ya mwaka mpya wa Kiirani yaani Nowruz imejawa na thamani kama vile amani, utulivu, umaanawi, uadilifu, matumaini, kujitolea muhanga na udugu. Amesema Obama hafahamu thamani hizi za kibinaadamu na kimaanawi wakati akitoa ujumbe wa Nowruz kwa taifa la Iran. Aidha rais wa Iran amewataja watawala wa Marekani kuwa vibaraka wa Utawala wa Kizayuni wa Israel. Amesema Iran haitilii maanani matamshi ya watawala wa Marekani.
Katika ujumbe wake wa Nowruz Obama aliilaumu serikali ya Iran kutokana na kile alichodai eti ni kampeni ya ukandamizaji baada ya uchaguzi wa rais Juni 2009. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Seyyed Ali Khamenei katika hotuba ya Nowruz Machi 22 aliukosoa ujumbe wa Nowruz wa Obama na kuwataja watawala wa Marekani kuwa wanafiki.
770514