IQNA

Maombolezo ya Bibi Fatima Zahra SA

11:35 - May 07, 2011
Habari ID: 2118126
Tarehe Tatu Jamadu Thani inasadifiana na siku ya kuuawa shahidi Bibi Fatima Zahra Salamullah Alaiha, Bintiye Mtume wa Uislamu SAW na mke mwenye kujitolea wa Imam Ali AS.
Ni mwanamke ambaye katika kipindi kifupi cha maisha yake, alikuwa chimbuko la baraka nyingi kwa ajili ya Waislamu na Uislamu. Jina la Fatima Salamullah Alaiha liliambatana na fadhila kama vile taqwa, elimu, kujitolea, ukarimu, ushujaa, ubora na ukamilifu. Tunachukua fursa hii kutoa salamu zetu za rambi rambi kwa mnasaba huu wa kumbukumbu ya kuuawa shahidi Bibi Fatima Zahra Salamullah Alaiha.
Salamu ziwe juu yako ewe binti wa Mtume wa Mwenyezi Mungu, salamu ziwe juu yako ewe Kiongozi wa Wanawake wa Dunia, salamu ziwe juu yako ewe ambaye Mwenyezi Mungu ana radhi naye na wewe ambaye unayeridhika na Mwenyezi Mungu. Salamu ziwe juu yako ewe mwenye fadhila na rahma na baraka.
Bibi Fatima Zahra Salamullah Alaiha baada ya kuaga dunia Mtume SAW aliishi katika dunia hii kwa muda wa takribani siku 90. Kuaga dunia Mtume kulikuwa msiba mkubwa kwa Waislamu hasa familia yake. Msiba huu uliandamana na masaibu mengi kwa Ahul Bayt wa Mtume SAW. Imenukuliwa kuwa baada ya kuaga dunia Mtume SAW, Bibi Fatima Salamullah Alaiha alilia sana. Lakini majonzi yake hayakuwa tu kwa sababu ya kuwa mbali na baba yake. Mwanamke huyu mtukufu alikuwa akitafakari kuhusu mustakabali wa Uslamu. Matukio ambayo yalikuwa yakijiri kwa sababu ya watu kuwa mbali na mafundisho ya wahyi yalivuruga itikadi zao. Sehemu ya msiba wa Fatima Zahra Salamullah Alaiha ulitokana na wanaadamu ambao hawakuwa wamepata muongozo wa kutosha. Kwa hivyo baada ya kuaga dunia Mtume SAW, Fatima Salamullah Alaiha alijaribu kuwabainishia watu ukweli ili kuzuia upotofu. Katika mkondo huu alitoa hotuba mbili muhimu na zenye thamani kubwa. Alitoa moja ya hotuba hizo katika msikiti wa Madina na nyingine akiwa miongoni mwa kundi la wanawake Muhajirina na Ansar.
Hotuba isiyo na kifani ya Bibi Fatima Salamullah Alaiha katika Msikiti wa Mtume SAW iligawanyika katika sehemu mbali mbali na kila kimoja ikiwa na lengo la kubainisha muongozo wa kufuatwa. Bibi Fatima Salamullah Alaiha katika hotuba zake kwa hadhirina alitoa mafundisho halisi kabisa ya mbinguni. Alibainisha masuala muhimu ya tauhidi, utume na kuchambua matukio baada ya kuaga dunia Mtume. Kubainisha itikadi za kidini na ubora wa maadili ni johari inayopatikana katika sehemu ya hotuba hii aliposema:
"Kwa hakika Imani kwa Mwenyezi Mungu ni chanzo cha utwahirifu na utakasifu wenu utakaokuwekeni mbali na shirki, sala itawaondolea kiburi na zakaa inapelekea kutakasika nafsi na kuongezeka rizki ya kila siku nayo saumu ni chanzo cha kudumu ikhlasi'.
Bibi Fatima Zahra Salamullah Alaiha katika hotuba hii aliashiria nukta muhimu kuhusu kile kinachoibua hitilafu na mgawanyiko miongoni mwa Waislamu. Alisema njia ya kujiepusha na mifarakano ni kufungamana na Ahul Bayt wa Mtume. Kuhusu hili alisema:
"Mwenyezi Mungu ameleta uimamu na uongozi wa Ahlul Bayt wa Mtume ili kuzuia aina yoyote ya ubinafsi na mifarakano na vile vile akafanya kuwa wajibu umoja ili chini ya kivuli hicho Waislamu waweze kupata salama ya dunia na akhera"
Bibi Fatima Zahra Salamullah Alaiha aliinukia na kulelewa katika chuo cha wahyi. Aliishi katika nyumba ambayo ilikuwa kituo cha mafundisho ya Mwenyezi Mungu na mahala pa kuteremshiwa aya za Qur'ani Tukufu. Kwa hivyo tokea utotoni alipata mafunzo ya kiwango cha juu zaidi ya maadili bora na umaanawi na yote hayo yanadhihirika katika tabia na mwenendo wa Baba yake, Mtume Muhammad SAW. Mtume SAW alisema katika hadithi: "Binti yangu Fatima ni kiongozi wa wanawake wa zama na vizazi vyote. Yeye ni sehemu yangu na ni tunda la moyo wangu. Yeye ni huri katika uso wa mwanaadamu. Kila wakati aliposimama katika mihrabu ya ibada mbele ya Mola wake muumba, nuru yake iliwaangazia malaika wa mbinguni kama ambavyo nuru ya nyota inavyoangazia ardhi". (Kutoka Kitab Amali cha Sheikh Mufid.
Ibada kwa mtazamo wa Bibi Fatima ilikuwa na upeo mpana na haikuishia tu katika sala na dua katika mihrabu.
Kumuabudu na kumhudumia Mwenyezi Mungu ni mambo yaliyokuwa mhimili wa kila kitu katika maisha ya Fatima Zahra Salamullah Alaiha.
Upendo na huruma ya Bibi Fatima Zahra Salamullah Alaiha kwa watu wa zama zake ni suala linalojitokeza wazi katika maisha yake. Sifa zake hizo zilienea miongoni mwa watu wote. Watu waliohitajia msaada ambao walikuwa wamepoteza matumani ya kusaidiwa sehemu zote walifika katika nyumba ya Fatima Salamullah Alaiha na hapo walipata msaada uliandamana na ukarimu wake.
Fatima Zahra Salamullah Alaiha alichukulia suala la kutoa msaada kwa wahitaji kuwa aina moja ya ibada. Alijua vyema kuwa Mwenyezi Mungu alifurahishwa na amali hiyo. Kwa mtazamo wa Mtukufu huyo mwanaadamu anaweza kuishi katika dunia na kufaidika na umaridadi wake hali ya kuwa moyo wake umezama katika mapenzi yasiyo na kikomo kwa Mwenyezi Mungu. Ni kwa sababu hii ndio siku moja alimwambia baba yake Mtume SAW: 'Ewe Baba yangu! Furaha ninayopata katika kumhudumia Mwenyezi Mungu inaniweka mbali na matakwa yote na ninapenda kushikamana na mtazamo maridadi na mzuri wa Mwenyezi Mungu."
Hakuna shaka kuwa ufahamu wa kina wa mwanamke huyo Mtukufu kuhusu uhusiano wa kimaanawi na Mola Muumba ni jambo lililomuwezesha kuvumilia masaibu na machungu yaliyompata maishani.
Maisha ya Bibi Fatima Salamullah Alaiha yalijawa na harakati ya kuleta mabadiliko katika itikadi potofu za kijahilia. Alikuwa kielelezo cha namna Mtume SAW alivyovunja mila potofu za kijahilia za kuwavunjia heshima wanawake na watoto.
Katika zama ambazo wasichana walikuwa wakizikwa hai, mikono ya Bibi Fatima ilikuwa sehemu iliyobusiwa na Mtume SAW. Moja ya nukta nyingine katika sira ya bibi Fatima Salamullah Alaiha ilikuwa ni kutojali vivutio vya dunia na kuishi maisha sahali. Tokea utotoni aliyatazama maisha kwa mtazamo wa kina. Salman Farsi anasema: 'Siku moja nilimuona Bibi Fatima Salamullah Alaiha akiwa amevaa baibui sahali na ya bei rahisi. Nilishangaa na kujisemesha mwenyewe kuwa mabinti wa mfalme wa Iran na Qeisar wa Roma wamekaa katika viti vilivyotengenezwa kwa dhahabu huku wakiwa wamevaa nguo ghali. Lakini binti wa Mtume wa Uislamu amevaa nguo na baibui sahali. Baada ya muda nilimsikia Fatima Salamullah Alaiha akisema: "Yaliyo dhahiri katika dunia hayanihadai. Mwenyezi Mungu amezihifadhi neema zake kwa watenda mema siku ya kiyama". Kuhusu thamani ya kufanya ibada kwa ikhlasi Bibi Fatima Zahra Salamullah Alaiha alisema: "Mtu anayemuabudu Mwenyezi Mungu kwa Ikhlasi, Mola Muumba atampa maslahi bora zaidi." (Biharul Anwar Jildi 67 Uk. 249. Bibi Fatima Zahra Salamullah Alaiha alisimama kidete kupinga dhulma na kutetea haki. Alikuwa kigezo cha kuigwa katika jamii kutokana na misimamo yake imara. Katika vipindi mbali mbali vya maisha yake kama mke, mama mlezi wa watoto hadi kutoa hotuba na kutetea haki, Bibi Fatima Zahra Salamullah Alaiha alinuia tu kumridhisha Mwenyezi Mngu. Kuaga dunia Mtume SAW kulimtia huzuni sana Bibi Fatima Salamullah Alaiha. Alikuwa na moyo laini sana. Hayo yakiandamana na maumivu aliyoyapata katika kumtetea mume wake, Imam Ali AS, ni mambo yaliyomfanya Bibi Fatima Salamullah Alaiha awe mgonjwa. Katika lahadha ya mwisho ya maisha yake, Bibi huyu mtukufu alijawa majonzi kutokana na watu ambao hawakutekeleza wasia wa Mtume wao. Akiwa katika hali hiyo aliomba maji na kushika wudhuu na kulala akiwa ameelekea Qibla. Maneno yake ya mwisho yalielekezwa kwa Mume wake, Imam Ali AS. Katika wasia wake alimuambia kuwa usiku ukiingia amuoshe josho la ghusl na amzike wala asimfahamishe yeyote. Wakati moyo malakuti wa Bibi Fatima Zahra Salamullah Alaiha ulipopaa kuelekea pepeoni, Ali AS kwa kimo kilichopinda kutokana na huzuni kubwa ya kuwa mbali na Zahra aliufungua moyo wake kwa kusema haya: "Kutengana na wewe ni jambo gumu sana kwangu na huu ni msiba ambao kutokana nao sitaweza kuridhika tena."
Kwa mara nyingine tunatoa salamu zetu za rambi rambi kwa mnasaba wa kumbukumbu ya kuuawa shahidi Bibi Fatima Salamullah Alaiha na tunamaliza makala hii kwa maneno ya mtukufu huyo aliposema: "Katika ulimwengu wenu ninayapenda mambo matatu. Kusoma Qurani Tukufu, kuuangalia uso wa Mtume wa Mwenyezi Mungu na kutoa kwa njia ya Mwenyezi Mungu." (Al Waqi'e al Ayam Khiyabani, Kitab as-Siyam uk. 295.

787373
captcha