Jamil Kheir Bahram, Waziri wa Masuala ya Kiislamu wa Malaysia amesema kuwa serikali ya nchi hiyo imechukua uamuzi wa kuanzisha vyuo vya Kiislamu vitakavyokuwa vikitoa masomo ya masuala ya kiuchumi na mifumo ya benki za Kiislamu nchini.
Akizungumzia suala hilo hapo jana Jumanne katika kikao cha ufunguzi wa duru ya 17 ya mkutano wa taasisi za kifedha za Kiislamu huko katika mji wa Putri Jaya, Waziri huyo amesema serikali ya nchi hiyo inashirikiana na Misri pamoja na Saudi Arabia kwa madhumuni ya kuanzisha nchini humo vyuo vikuu vitakavyotoa masomo ya kitaalamu kuhusiana na mifumo ya benki na uchumi wa Kiislamu. Amesema lengo kuu la kuanzishwa vyuo hivyo ni kukidhi haja ya Malaysia ya daima kuwatumia wasomi wake wa ndani katika nyanja mbalimbali zikiwemo za masuala yanayohusiana na sheria za Kiislamu, miamala ya kifedha na mifumo ya benki na uchumi wa Kiislamu. Amesema hadi sasa serikali ya Malaysia imefanya juhudi kubwa kufikia lengo hilo ikiwa ni pamoja na kuwatuma wanafunzi 63 nchini Misri kwa shabaha ya kusomea uchumi wa Kiislamu. 802670