IQNA

Jumba la makumbusho ya kale kuanzishwa Najaf

21:11 - June 11, 2011
Habari ID: 2136312
Kamati ya Turathi za Kiutamaduni na Athari za Kihistoria ya mji mtakatifu wa Najaf huko Iraq itaanzisha jumba la makumbusho na athari za kihistoria na mambo ya kale katika mji huo.
Hatua hiyo ni katika mikakati ya kutekeleza mpango wa Najaf, mji mkuu wa kiutamaduni wa ulimwengu wa Kiislamu mwaka 2012.
Kituo cha habari cha Alnajafnews kimeripoti kuwa Kamati ya Turathi za Kiutamaduni na Athari za Kihistoria ya mji mtakatifu wa Najaf imeazimia kujenga jumba hilo la makumbusho kwa shabaha ya kusajili athari za kihistoria za mji huo mtakatifu na kuhakiki umri wa athari hizo.
Kamati hiyo imetenga dinari bilioni nne za Iraq kwa ajili ya kununua athari za kale za kipindi cha kabla ya kuundwa serikali ya zama hizi huko Iraq.
Mkuu wa Kamati ya Turathi za Kiutamaduni na Athari za Kihistoria ya mji mtakatifu wa Najaf Nazzar al Naffah amesema jumba hilo litajengwa katika moja ya maeneo ya kihistoria ya mji mtakatifu wa Najaf na kwamba nyaraka na athari zote za mji huo zitakusanywa katika jumba hilo.
Mji mtakatifu wa Najaf mbali na kuwa na haram na kaburi la Imam Ali bin Abi Twalib (as), lina maeneo mengi ya kihistoria ambayo kila moja linaakisi matukio muhimu ya historia ya Iraq. 806700
captcha