Ayatullah Ali Khamenei ambaye amehutubia mjumuiko huo amesema kuwa kuwapo vipawa vikubwa na tajiri kati ya malenga hapa nchini ni bishara ya kurejea kipindi cha kuchanua na kung'ara kwa mashairi. Ameongeza kuwa katika mustakbali wa hivi karibuni tutashuhudia ustawi mkubwa wa sanaa ya mashairi hapa nchini kutokana na kuimarika zaidi vipawa vya washairi vijana.
Ameashiria uwanja mzuri wa mashairi ya kidini kwa ajili ya kutumia vipawa na neema waliyopewa washairi na kusema shukrani ya washairi kwa neema hiyo ya Mwenyezi Mungu ni kutunga mashairi yenye maana za kina na thamani aali na kuwa kalibu na chombo bora cha kueleza na kubainisha maarifa ya Mwenyezi Mungu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewausia wasomaji wa tungo za kuwasifu Ahlul Baiti wa Mtume Muhammad (saw) kusoma mashairi yenye mafunzo ya maadili mema, maarifa na masuala la kiirfani na kiroho katika mikusanyiko ya wananchi na vijana. Amesema kuwa tungo kama hizo hutia nuru na mwanga katika nyoyo na kuzusha mapinduzi ya kiroho ndani yake. Amesisitiza kuwa mashairi kama hayo pia huzidisha uwezo wa kifikra wa wasikilizaji wake na kwamba huo ni wadhifa na kazi ya jamii ya wasomaji tungo hizo.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa dua ni uwanja mwingine nzuri kwa ajili ya kuweza kutunga mashairi ya kidini. Ameongeza kuwa maana bora zaidi kwa ajili ya kutunga mashairi ya dua na maombi zinaweza kutolewa katika dua kama zile zinazopatikana katika kitabu cha Sahifa Sajjadiyyah na iwapo washairi hodari na vijana hapa nchini wataanisika na dua hizo basi hapana shaka watafanikiwa kutunga mashairi ya hali ya juu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameitaja dua ya siku ya Arafa ya Bwana wa Mashahidi Imam Hussein bin Ali (as), dua ya Imam Zainul Abidin maarufu kwa jina la Abu Hamza al Thumali na Ziara ya Jamia' kuwa ni vyanzo vizuri kwa ajili ya kutunga mashairi ya dua, maombi na matukufu ya Ahlul Bait (as). Ameongeza kuwa mashairi ya kidini yana uwezo mkubwa wa kuathiri fikra za wasikiliza na malenga hodari anaweza kukata kiu ya kupata maarifa safi ya roho ya msikilizaji wake kwa kutumia maarifa aali ya Uislamu na tauhidi yaliyomo ndani ya Qur'ani na Nahjul Balagha.
Ayatullah Khamenei pia amewausia malenga hao mambo kadhaa ikiwa ni pamoja na kuyapa mashairi yao maana za kina kwa ajili ya kueleza jambo fulani kwa kutumia fani ya sanaa, kuchagua misamiati inayofaa, kuchunga kanuni za lugha na fasihi na kutilia maanani zaidi masuala ya Mapinduzi ya Kiislamu hususan vita vya kujitetea kutakatifu.
Amesisitiza pia juu ya udharura wa kuimarishwa zaidi uhusiano kati ya washairi wa masuala ya kidini na akasema: "Nyinyi vijana wenye imani na mnaowapenda Ahlul Bait wa Mtume (saw) mnapaswa kulinda mvuto na mapenzi yenu kwa watukufu hawa na kudumisha njia hiyo kwa kuwa macho daima."
Ayatullah Ali Khamenei ametilia mkazo suala la udumishaji wa kifikra wa hamasa ya kipindi cha kujitetea kutakatifu na ikhlasi ya wakati huo na akasema washairi ni miongoni mwa watu wanaobeba amana na wanalazimika kulinda na kukabidhi amana hiyo ya ikhlasi na masuala hayo ya kiroho. 809377